SPIKA ATAKA BENKI ZISAIDIE UCHUMI KWA MIKOPO, KUPUNGUZA RIBA


Spika wa Bunge, Anne Makinda amesema ili sekta ya benki itoe mchango wake kikamilifu katika kukuza uchumi wa Taifa, ni muhimu kwa benki hizo kurahisisha masharti ya mikopo pamoja na kupunguza viwango vya riba ambavyo kwa sasa viko juu mno. 
Makinda aliyasema hayo juzi mjini hapa wakati akizindua Tawi la Benki ya NMB la Bunge, uzinduzi uliohudhuriwa na Naibu Waziri wa Fedha, Adam Malima, Ofisa Mtendaji Mkuu wa benki hiyo, Mark Wiessing na Mwenyekiti wa Bodi, Profesa Joseph Semboja. 
Alisema huduma zenye ubora na za kisasa za kibenki ni muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi nchini. 
“Hata hivyo, ili sekta ya benki iweze kutoa mchango wake kikamilifu katika kukuza uchumi wa Taifa ni muhimu kwa benki hizo kurahisisha masharti ya mikopo kwa wateja wake sambamba na kupunguza viwango vya riba kwa wakopaji ambavyo kwa sasa ni vya juu mno,” alisema Makinda. 
Alisema kupunguza masharti ya mikopo na viwango vya riba kutaongeza hamasa ya kujiwekea akiba miongoni mwa Watanzania, na wakati huo huo kuongeza idadi ya Watanzania wanaotumia huduma za kibenki kwani idadi hiyo kwa sasa ni ndogo sana. 
Awali, Ofisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Wiessing alisema NMB Tawi la Bunge, ni tawi la 153 nchini, huku wakiwa wameongeza matawi 53 tangu kubinafsishwa miaka 10 iliyopita.  Alisema wataongeza matawi mengine 17 kufikia mwisho wa mwaka huu na kufikisha matawi 170.

No comments: