SITTA AONYA IKIVUNJIKA EAC MADHARA YATAKUWA MAKUBWAWizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki imesema Tanzania haina tatizo na nchi yoyote katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na ipo tayari kuingia katika Shirikisho, lakini haitakurupuka katika maamuzi yoyote.
Hatua hiyo inatokana na kuwa ikiwa jumuiya hiyo itavunjika tena, madhara kwa Tanzania ni makubwa kuliko nchi nyingine yoyote, kwa kuzingatia madhara iliyopata ilipovunjika jumuiya ya awali.
Waziri wa Wizara hiyo, Samuel Sitta alisema hayo juzi jioni wakati akifanya majumuisho ya hotuba yake ya bajeti pamoja na kujibu hoja mbalimbali zilizotolewa na wabunge.
Alisema uhusiano huo ulipovunjika mwanzo, uliiacha Tanzania katika sintofahamu kwa sababu ofisi muhimu zilikuwa nje.
Sitta alifafanua kuwa wakati jumuiya hiyo ilipovunjika mwaka 1977, ofisi za Shirika la Posta na Simu zilikuwa Uganda wakati za Bandari zilikuwa Kenya.
Alisema hatua za kiuangalifu, zinazochukuliwa na Serikali ni nzuri  na kufanya kwa uangalifu ambayo mara nyingi Tanzania inaonekana iko sahihi kwa misimamo hiyo.
Awali, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni, Freeman Mbowe alihoji iwapo Serikali ina nia ya dhati ya kuingia katika shirikisho hilo, kutokana na kuonekana ni kikwazo katika kuelekea hatua mbalimbali.
Awali, akizungumzia kuhusu mahusiano  baina ya  Rwanda na Tanzania alisema ni mazuri tu na kwamba suala la uhasama baina ya nchi hizo linakuzwa na vyombo vya habari.
Akifafanua kuhusu mikutano iliyozishirikisha nchi za Uganda, Rwanda na Kenya na kuitenga Tanzania na Burundi, Sitta alisema hatua ile isiwatie wasiwasi Watanzania kwani hata mwaka huu Tanzania, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC) watafanya mkutano wao wa nchi za Afrika ya Kati.
Katika hatua nyingine, Waziri Sitta alimshukuru Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema) kwa kutoa ushauri mzuri wa kimaandishi, kuhusu maandalizi ya sera ya mtangamano wa Afrika Mashariki na kuahidi kuufanyika kazi.
Alieleza  kuwa wizara inaendelea  kutoa elimu kwa Watanzania, ambapo hadi sasa wizara hiyo imefanikiwa kutoa elimu katika maeneo yote ya mipakani kuhusu shirikisho hilo na inaendelea katika maeneo mengine.
Awali, Mbunge wa Longido, Michael Laizer (CCM)  alihoji wizara imejiandaaje kutoa elimu kwa Watanzania hususan wa mipakani, kwa sababu wengi wao hawana elimu kuhusu shirikisho hilo.
Aidha, Laizer alisema uzoefu unaonesha kuwa raia wa Kenya, wameelimishwa ipasavyo ndiyo maana wamekuwa wakichangamkia biashara hapa nchini na kwamba wanafanya bila bughudha yoyote, ukilinganisha na Watanzania wanaoghasiwa kwa kiwango kikubwa wawapo nchini Kenya.

No comments: