SITA MBARONI WAKIHUSISHWA NA KUNDI LA MBWAMWITU DARJeshi la Polisi limewakamata watu 6, wanaosadikiwa kuwa ni vinara wa vikundi hatari vya `Mbwa Mwitu’, `Watoto wa Mbwa’ au `Panya Road’ .
Vikundi hivyo vinajihusisha na matukio ya kihalifu jijini Dar es Salaam.
Vijana wanaounda makundi hayo, wengi wakiwa wenye umri wa kati ya miaka 16 na 20, hutembea kwa makundi na kufanya uhalifu kwa kutumia silaha, kama mapanga, visu, nondo na marungu.
Hayo yalisemwa na Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleman Kova wakati akizungumza na waandishi wa habari jana.
Alitaja waliokamatwa wakihusishwa na vikundi hivyo kuwa ni Athuman Said (20), mkazi wa Kigogo, Joseph Ponela ambaye ni dereva bodaboda, Clement Peter (25) fundi seremala, Roman  Vitus (18) mfanyabiashara, Mwinshehe Adam (37) mkazi wa Temeke na Daniel Peter (25) mkazi wa  Yombo.
Alisema Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limefanya msako katika maeneo mbalimbali ya Jiji ili kudhibiti makundi ya uhalifu na vijana wahuni wasio na kazi.
Aliongeza kuwa maeneo ambayo yameonekana kuwa na vijana hao ni Kigogo, Magomeni, Tabata, Manzese na Mbagala.
"Askari wa kutosha wa doria wamepangwa kufanya doria ili kuthibiti milipuko yoyote ya vitendo vya kihuni vinavyoleta hofu kwa wananchi," alisema Kova.
Aidha, alisema kumekuwa na mtindo wa watu ambao hawafahamiki jijini hutuma ujumbe mfupi wa simu za mkononi, wakieneza uvumi kwamba maeneo yao yamevamiwa na makundi ya Mbwa Mwitu au Panya Road.
Alisema uvumi huo, ulianza Mei 18 na 20 mwaka huu baada ya vibaka wawili wa kundi hilo, kuuawa na hofu ilikuja baada ya mazishi ya vijana hao, kwani wangeweza kulipiza kisasi.
"Jeshi la Polisi linatoa onyo kali mtindo huu ukome, kwani watu hao wanasababisha hofu kwa wananchi," aliongeza Kova.
Alisema Jeshi la Polisi limejiimarisha kiulinzi na vijana hao, hawana uwezo wa kufanya watakavyo, kama uvumi unavyoenezwa kimakosa.
Jeshi la Polisi limeamua kufanya msako huo baada ya kundi la Panya Road, kuibuka wiki hii na kusababisha hofu kwa wananchi wengi, ikiwa ni pamoja na kufanya uporaji na kujeruhi kwa kutumia silaha za jadi, kama marungu, mapanga, visu na nondo katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam.

No comments: