SIMON GROUP WASHANGAA UPOTOSHAJI WA MNYIKA



Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Simon Group inayoendesha Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA), Robert Kisena ameeleza kushangazwa na upotoshaji uliofanywa na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika juu ya uhalali wa umiliki wa hisa za shirika hilo.
Pamoja na kushangazwa na upotoshaji huo, Kisena amesema Mnyika ni miongoni mwa wajumbe wa Baraza la Madiwani wa Jiji la Dar es Salaam walioshiriki katika vikao halali vilivyojadili hatua zote za kuuza hisa kwa Simon Group.
Mbali ya upotoshaji huo kulenga kulihujumu Shirika la UDA, Kisena alisema una lengo pia la kuwahujumu wananchi wa Dar es Salaam, kuhujumu uchumi wa Taifa, lakini pia  umewashitua wadau wanaofanya kazi na Simon Group kuiboresha UDA zikiwemo taasisi  za fedha, wasambazaji wa mabasi na wataalamu kutoka nje. 
Kisena aliyasema hayo Dar es Salaam jana alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu uendeshaji wa UDA, siku chache baada ya Mnyika kutoa madai mazito bungeni akiishutumu Serikali kwa kile alichosema imefumbia macho ufisadi aliodai umefanywa katika uuzwaji wa hisa za UDA kwa Simon Group.
Mnyika alisema pia anashangazwa na uwepo wa Simon Group kwenye shughuli za uendeshaji wa UDA na kuitaka Serikali kutaifisha mabasi yote ili kuzuia UDA chini ya Simon Group kuendelea kutoa huduma za usafiri katika Jiji la Dar es Salaam.
Kisena akizungumzia madai hayo ya Mnyika alisema; “Nimeshangazwa sana na maneno haya ya Mnyika bungeni na nimeridhika kusema kuwa Mbunge huyu anatumiwa na  mfanyabiashara mmoja (jina linahifadhiwa) ambaye tangu 2011 amekuwa akiendesha mbinu chafu za kuichafua Simon Group.
“Ni jambo la kusikitisha kuona pamoja na jitihada za kufanya uwekezaji mkubwa wa zaidi ya Sh bilioni 300 ili kuwaondolea tabu ya usafiri watu wa Dar es Salaam, Mbunge wa Jimbo la Dar es Salaam anatumika katika kuwahujumu wananchi wake, jambo linalosikitisha.”
Akizungumzia madai ya Mnyika kuhusu kuwepo kwa ufisadi UDA, Kisena alisema madai hayo si mapya kwani yalikuwepo tangu mwaka 2011 hatua iliyosababisha Serikali Kuu kuagiza wanahisa wa wakati huo, Simon Group, Msajili wa Hazina na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kukutana na kujadiliana.
“Kutokana na maelekezo hayo ya Waziri Mkuu, tulikutana Novemba 15, 2011 na kujadili malalamiko yote yakiwemo kwamba Simon Group tumeuziwa UDA kwa bei ndogo. Baada ya majadiliano ya kina ilikubalika kuwa pamoja na mambo mengine ufanyike upya uthamini wa bei ya hisa tulizonunua.
“Pamoja na kuzungumzia hayo tulizungumzia pia namna ya kumaliza migogoro ya UDA, kurekebisha kasoro zilizokuwa zinajitokeza katika uendeshaji wa shirika ili kuleta tija na ufanisi si kwa kuliua shirika bali kwa kuliboresha na kulistawisha zaidi.
“Kwa kauli moja wanahisa wote tukakubaliana UDA kuendeshwa na Simon Group na tukakubaliana kuwa na Bodi ya Wakurugenzi ya pamoja ambapo Januari 9, 2012, Jiji walimteua Mbunge wa Ukonga, Eugene Mwaiposa kuwa mjumbe wa Bodi katika kikao ambapo Mnyika alishiriki, na wakati huo Serikali iliendelea kufanya uthamini upya wa bei ya hisa za ununuzi kupitia Kampuni ya KPMG,” alisema.
Kisena alisema ilipofika Agosti 16, 2013, wanahisa hao wa UDA waliitwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Serikali za Mitaa chini ya Mwenyekiti wake, Dk  Hamis Kigwangalla katika Ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam na kuzungumzia madai ya utata juu ya UDA.
“Baada ya maelezo na ufafanuzi wetu lakini Kamati ya Bunge ilituita Dodoma sisi sote ili kujadili zaidi suala la uendeshaji wa UDA, lakini walituagiza kuwa kabla ya kwenda Dodoma kifanyike kikao cha wadau wote muhimu wa UDA chini ya Mkuu wa Mkoa ili tuweze kuandaa taarifa ya pamoja juu ya mgogoro wa UDA na ufumbuzi wake.
“Tulifanya kikao hicho Agosti 28, 2013 tukiwa sisi sote Msajili wa Hazina, Jiji, Kampuni Hodhi ya Mashirika ya Umma (CHC) na Simon Group, ambapo katika kikao kile, Jiji walikuja na muhtasari juu ya kikao chao walichokaa Agosti 22, 2013  Mnyika akiwa mmoja wa wajumbe ambapo walifikia maazimio mbalimbali.
 “Miongoni mwa maazimio yao ni kuamua kuiuzia Simon Group hisa zake  3,631,046 kwa takribani  Sh bilioni 6 ili kufanya shughuli za UDA kusimamiwa kwa ubora zaidi na wao kupeleka nguvu zao kwenye Mradi wa Mabasi ya Haraka (DART). Hazina pia walikuja na maazimio ya kuiachia uendeshaji wa UDA Simon Group.
“Baada ya kikao hicho tuliandika taarifa ya pamoja ya ni mambo yapi tumeyapatia ufumbuzi na nini hatma ya baadaye ya UDA. Katika majadiliano hayo yote tulizingatia pia taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) anazosema Mnyika, na hivyo taarifa hizo za CAG pia si ngeni,” alisema.
Kisena alisema Agosti 31, 2013 na Septemba 1, 2013, kilifanyika kikao cha pamoja baina ya wanahisa wa UDA na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Serikali za Mitaa kikiwashirikisha pia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), watendaji wakuu wa Jiji la Dar es Salaam, Hazina na CHC.
“Kutokana na majadiliano yetu, Kamati iliamua kuwa migogoro yote iishe na migogoro ya bei ya hisa irekebishwe lakini iliagiza kuwa hayo yote yafanyike huku ikimpa mamlaka Simon Group kuendelea na uwekezaji kwa kuzingatia sheria ya uanzishwaji wa UDA. Utekelezaji wa maagizo ya Kamati umefanyika na hakuna tena utata katika UDA kama Mnyika anavyojaribu kuendelea kutumika kupotosha.”
Kisena akizungumzia madhara yaliyopatikana na taarifa hizo alisema ni pamoja na wadau wanaoshirikiana na Simon Group katika kuiboresha UDA zikiwemo taasisi za fedha, wataalamu na watengenezaji wa mabasi kuingiwa na shaka isiyo na sababu wala tija.
“Unajua wadau kama hawa unapoingia makubaliano nao ili kushirikiana katika uendeshaji wa mradi wenye mtaji mkubwa kama ilivyo sasa kwa UDA ni lazima uwajengee imani fulani ili waamini kwamba fedha zao au ushirikiano wao ni salama.Waliposikia habari za Mnyika walituandikia barua kuomba ufafanuzi, jambo ambalo si zuri sana,” alisema.
Alisema mbali ya madhara hayo, yapo madhara kwa wananchi wa Jiji la Dar es Salaam wakiwemo wa Jimbo la Ubungo kuingiwa na hofu ya shirika lao wanalolitegemea sasa kwa usafiri likifika katika maeneo yote ya jiji na kwa saa zote hadi usiku kufa.
“Huyu ni Mbunge ambaye hajali maslahi ya wananchi wake, maana anaposema mabasi ya UDA yakamatwe na yasitoe huduma na Simon Group wafukuzwe maana yake ni kwamba  anashabikia uwekezaji mkubwa wa usafiri kama wa UDA wenye thamani ya Sh bilioni 300 ufe kwa kile anachodai kuwa anatetea Sh bilioni 11 zisipotee.
“Sisi UDA pamoja na kutoa huduma za usafiri tunachangia pia kwenye huduma nyingine za jamii kama kuchangia madawati na hata kuwasafirisha wanafunzi kwenda shule zilizo mbali zikiwemo za Ubungo, ndio maana nasisitiza kuwa kuna mazingira ya rushwa katika harakati hizi za Mnyika,” alisema Kisena.
Hali ya uwekezaji ilivyo
Kisena alisema madai kuwa Serikali imeuza hisa zake zote si sahihi kwa vile hisa za serikali 3,488,651 sawa na asilimia 23.26 zipo kama zilivyokuwa awali ingawa sasa zimepanda thamani kutokana na kuongezeka kwa uwekezaji jambo ambalo ni faida kwa Serikali.
Alisema kwa upande wa Simon Group sasa ina hisa 11,011,349 baada ya awali kununua hisa 7,888, 303 ambazo ziliongezwa bei baada ya kudaiwa kununuliwa kwa bei ya chini, lakini baadaye ikanunua tena hisa 3,631,046 zilizokuwa za Halmashauri ya Jiji.
Alisema mipango ya uwekezaji inaendelea vizuri kukiwa na lengo la kuwezesha UDA kuwa na mabasi 2,000 hadi mwisho wa mwaka huu na kwamba kwa sasa mabasi 300 yapo barabarani huku 200 yakiwa kwenye karakana kwa kufanyiwa maandalizi.
“Mabasi 1,500 yataendelea kuingia nchini kwa mabasi 300 kila mwezi na kimsingi haya ni kama tumeshayalipia maana tumeshafanya oda. Alisema mabasi marefu 50 yataingizwa nchini muda mfupi ujao na yatatoa huduma katika barabara za Nyerere, Bagamoyo na Kilwa.

No comments: