IRINGA YAPIGWA 'STOP' KUJENGA STENDI IGUMBILO

Serikali imefanya uamuzi mgumu kwa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kuzuia mpango wake wa kujenga stendi mpya ya mabasi ya mikoani katika eneo linalolalamikiwa na wadau wa mazingira la Igumbilo, mjini hapa.
Pia, imeipoza halmashauri hiyo kwa kuwaahidi kuchangia gharama mbalimbali zitakazohitajika kufidia na kutathimini eneo mbadala watakalopata kwa ajili ya ujenzi huo.
Zuio hilo lilitolewa jana mjini hapa kupitia matamko yaliyotolewa na mawaziri watatu tofauti, akiwemo Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe, Waziri wa Mazingira, Dk Binilith Mahenge na Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia.
Kwa pamoja walitoa ufafanuzi wa zuio hilo wakati wakizungumza na wanahabari ambao awali walizuiwa kuingia kwenye kikao kilichokuwa kikipokea taarifa hiyo.
Mbali na mawaziri hao, uongozi wa mkoa huo akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Iringa, wawakilishi wa vyama mbalimbali vya siasa, Baraza la
Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na wadau mbalimbali wa mazingira na maji walihudhuria kikao hicho.
Akitoa taarifa ya zuio hilo, Ghasia alisema tathimini ya pili ya athari ya mazingira iliyofanywa na NEMC inahalalisha uamuzi huo baada ya wizara ya maji kupinga ujenzi huo katika eneo hilo linalopitiwa na mto Ruaha Mdogo.
Waziri Ghasia alisema mto huo ndiyo chanzo pekee kinachohudumia jamii nzima ya wananchi wa manispaa ya Iringa na hivyo kujenga stendi jirani yake kutaongeza shughuli za kibinadamu zinazoweza kuathiri mto huo, mazingira yake na hatimaye wanufaika wake.
Kupitia Mamlaka ya Maji Safi na Majitaka Iringa (IRUWASA), serikali imewekeza katika mto huo zaidi ya Sh bilioni 70 ili kuwapatia wananchi maji safi na salama kupitia mradi ulizinduliwa na Rais Jakaya Kikwete Machi 22, 2012.
“Kwa hiyo tumewaeleza rasmi ndugu zetu wa manispaa kwamba stendi hiyo haitajengwa katika eneo hilo lakini kwa kuwa wanayo mipango ya ujenzi huo kwa ufadhili wa na Benki ya Dunia, watafute sehemu nyingine,” alisema.
Alisema serikali inatambua gharama ambazo manispaa hiyo imeingia tangu ianze mchakato huo mwaka 2008 na ili kuponya machungu hayo itawajibika kutoa fedha zitakazohitajika kwa ajili ya kuandaa eneo mbadala.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa, Amani Mwamwindi alikataa kutoa mtazamo wake baada ya kupokea uamuzi huo, hata hivyo Waziri Ghasia aliingilia kati na kuitaka halmashauri hiyo iendelee na mipango ya kujenga stendi kwa kutafuta eneo lingine.
Kwa ufadhili wa Benki ya Dunia, manispaa hiyo ilikuwa itumie zaidi ya Sh bilioni nne kukamilisha ujenzi wa stendi hiyo.

No comments: