SERIKALI YATETEA TUZO YAKE KWA JAJI WARIOBA

Nishani ya  Kuuenzi Muungano aliyopewa Jaji Joseph Warioba, haikumaanisha kumkejeli,  bali amepewa kwa heshima kama ilivyo kwa viongozi wengine waliopewa nishani hiyo.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Assah Mwambene, alisema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari,  kuhusu upotoshaji unaofanywa na baadhi ya vyombo vya habari.
Mwambene alisema Serikali haina ugomvi na Jaji Warioba na pia inamheshimu sana.
"Kuna baadhi ya taarifa zina mkanganyiko, zinaonesha kama Serikali imempa nishani Jaji Warioba kwa kumkejeli, jambo ambalo si kweli, Serikali inamheshimu," alisema Mwambene.
Alisema nishani aliyopewa Jaji Warioba, haihusu mchakato wa Katiba, ambao kuna baadhi ya taarifa za mchakato huo, ambazo zimekuwa zikieleza kuwa baadhi ya wajumbe wanamtukana Jaji Warioba.
"Serikali imempa nishani kwa sababu anastahili, wala haihusu mchakato huu wa Katiba, hata kama mtu anakinzana na Rasimu ya Jaji Warioba haimaanishi kamtukana, bali katoa mawazo yake na iliyopo ni rasimu na si Katiba," alisema.
Mwambene alisema kuwa nishani hiyo, mbali na Jaji Warioba, pia ilitolewa kwa viongozi wengine akiwamo aliyekuwa Waziri Mkuu, Fredrick Sumaye kama heshima ya kuuenzi Muungano.

No comments: