SERIKALI YASEMA UDA NI 'MALI YA UMMA'Hadi sasa mmiliki halali wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) ni Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na Serikali kupitia Msajili wa Hazina.
Naibu Waziri wa Fedha, Adam Malima alisema hayo jana bungeni na kuongeza kuwa Serikali iliondoa kesi mahakamani ya watuhumiwa wa UDA, ili kuruhusu uchunguzi kufanyika upya.
Alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema), Mdee alitaka kauli ya Serikali kuhusu utata wa utaratibu uliotumika katika uuzwaji wa hisa za Serikali katika Shirika hilo.
Pia alitaka kujua nani mmiliki halali wa hisa hizo kwa sasa pamoja na mgawanyo wa hisa kwa wamiliki hao.
Malima alisema hisa ndani ya Shirika la UDA hazijauzwa, mgawanyo wa hisa halali ni kama ulivyosajiliwa kwa msajili wa makampuni, kwa maana ya Halmashauri ya Jiji asilimia 51 na Serikali kupitia Msajili wa Hazina asilimia 49.
Naibu Waziri alisema mwaka 2006 Serikali iliamua kuuza hisa zake kwa asilimia 49 ili kupata mwekezaji mahiri mwenye uwezo wa kuliboresha shirika hilo.
Hata hivyo alisema Tume ya Kurekebisha Mashirika ya Sekta ya Umma  (PSRC) ilishindwa kumpata mwekezaji aliyekidhi vigezo vilivyowekwa.
Januari 2010 kwa mujibu wa Malima, Bodi ya UDA iliiarifu Serikali kuwa amepatikana mwekezaji ambaye ni Kampuni ya Simon Group ambayo ingeuziwa hisa za Serikali pamoja na hisa 7,880,303 ambazo hazikugawiwa wakati UDA inaanzishwa.
Malima alisema Serikali iliagiza Bodi kusitisha mpango wa kuizuia Simon Group Limited hisa zozote kutokana na kukiukwa kwa taratibu na misingi ya Sheria.
Akiuliza swali la nyongeza, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema) alitaka kupata kauli ya Serikali kuhusu kampuni hiyo kuendelea kumiliki na kuendesha Kampuni ya UDA sasa.
Mbunge huyo alisema Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) alishafanya uchunguzi kuhusu uuzwaji wa hisa za UDA na kubaini  kuwepo kwa ufisadi.
Alisema ripoti hiyo iliwasilishwa kwa Waziri Mkuu Machi 30 mwaka 2011, ambapo ilibaini ufisadi wa kutisha na kutaka Serikali itoe kauli baada ya kubaini ufisadi huo.
Aidha Mnyika aligusia kitendo cha Mwendesha Mashitaka wa Serikali (DPP), kuwasilisha hati mahakamani kutaka watuhumiwa wote wa UDA waachiwe kwa kuwa hawana kesi ya kujibu.
Mnyika alisema bila majibu watazidi kuamini kama Serikali ya CCM inawalinda vigogo ambao ni mafisadi.
Akijibu hoja ya Mnyika, Malima alikiri kuwepo kwa utata kwa mazingira ya uuzwaji wa UDA kutoka pande zote mbili za umiliki yaani Serikali na Halmashauri ya Jiji. 
Alisema baada ya CAG kutoa ripoti yake ilielezea ukiukwaji   wa taratibu na sheria za uuzwaji, ndipo DPP aliamua kuondoa kesi mahakamani ili uchunguzi uendelee.
Malima alisema sasa vyombo vya uchunguzi ikiwemo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) vinaendelea na uchunguzi dhidi ya ufisadi uliobainishwa na CAG.

No comments: