SERIKALI YAKANUSHA KUTOHUDUMIA MIKOPO MIFUKO YA HIFADHI

Mikopo inayotolewa na Mifuko ya Hifadhi za Jamii nchini kwa serikali nchini  inatolewa baada ya kudhibitishwa na Benki Kuu (BoT) na SSRA ambayo pia inasimamia ulipwaji wake ambao serikali inaendelea kulipa.
Ilielezwa kuwa siyo kweli kuwa serikali hailipi mikopo hiyo, kwani malipo yanaendelea vema na inayotokea ni ucheleweshwaji na siyo kutolipa kabisa.
Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Makongoro Mahanga aliliambia bunge juzi wakati akihitimisha majadiliano ya bajeti ya wizara hiyo.
Alisema serikali inaendelea kulipa madeni hayo yakiwemo ya ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), daraja la Kigamboni, nyumba na majengo ya polisi na miradi mingine mbalimbali.
“Serikali inalipa chini ya uchunguzi wa SSRA na Benki Kuu ambao hata ikichelewa katika ulipaji inakumbushwa kama ilivyo kwa wakopaji wengine,” alisema Mahanga.
Alisema mikopo hiyo hutolewa kulingana na miongozo ya uwekezaji ya mwaka 2012, hivyo uwekezaji na ukopaji katika mifuko hiyo inafanya vizuri na faida zinaonekana.
Pia, Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudentia Kabaka alikanusha taarifa iliyotolewa bungeni hapo kuwa Shirika la Hifadhi za Jamii la NSSF lipo katika hatari ya kufilisika na kusema haipo wala haitarajii.
Alisema tathmini kuhusu mfuko huo iliyofanywa na kampuni ya Canada ilionesha NSSF ina uwezo wa kujiendesha kwa usalama bila matatizo kwa miaka 50 ijayo.
Alisema pia ina uwezo wa kulipa mafao kwa asilimia 78 tofauti na asilimia 60 ambayo ni ya kimataifa  huku akibainisha kuwa hakuna uwekezaji wowote unaofanywa na mifuko hiyo ya hifadhi ya jamii bila kudhibitishwa na Benki Kuu na SSRA.
Huku akieleza bayana kuwa changamoto iliyojitokeza katika ulipaji mkopo wa ujenzi wa Machinga Complex, serikali inaangalia namna nyingine ya kuanza kulipa mkopo huo.

No comments: