RUKSA KUIKEMEA SERIKALI INAPOKOSEAWaziri Mkuu, Mizengo Pinda amesema ruksa wabunge kukemea Serikali inapokosea lakini wasiikatishe tamaa katika mambo mazuri inayoyafanya badala yake waipe moyo. 
Kauli hiyo aliitoa wiki hii bungeni alipokuwa akihitimisha michango ya wabunge waliochangia  kuhusu bajeti ya mwaka wa fedha wa 2014/15 ya ofisi yake. 
Kauli hiyo ilikuja kutokana na baadhi ya wabunge hususani wa upinzani, katika uchangiaji kubeza na kuponda  baadhi ya mambo yaliyofanywa na Serikali ikiwemo barabara zilizojengwa kwa kusema hazina ubora.
“Unafika mahali unasema, Mungu wangu nifanyeje. Lakini tutaendelea na hizo juhudi. Tumeshajifunza, wakati mwingine kulaumiwa umiwa ndiyo sehemu ya mambo ilivyo, tusikate tamaa,”  alisema Pinda.
Aliendelea kusema, “Naendelea kuwaomba wabunge, muendelee kuunga mkono juhudi hizi. Tukemeeni pale mnapoona tunakosea.  Mimi sina ugomvi na hilo. Lakini msitukatishe tamaa, tutie moyo ili tuweze kufanya vizuri zaidi,” alisema Pinda. 
Pinda katika ufafanuzi alitoa takwimu mbalimbali kwa wabunge kuonesha juhudi za Serikali katika kufanikisha maendeleo, hususani kwenye kilimo, nishati, miundombinu na pato la wananchi na kusema upo uhakika ifikapo mwaka 2025, Tanzania itakuwa  na uchumi wa kati. 
Alisema mwaka 2000 barabara za la lami zilikuwa kilometa 3,900. Uongozi wa awamu ya tatu ulianzisha  miradi 14 yenye  kilometa 1,226  na ikamudu kumaliza miradi saba. Awamu ya nne  ilipoingia ilirithi miradi iliyobaki.   
Pia chini ya awamu ya nne, ilianzishwa miradi mipya 26 sawa na kilometa 1,759 ambazo kati yake, kilometa  1,270.8 sawa na asilimia 72, zimekamilishwa kwa kiwango cha lami na kubaki kilometa 488 ambazo Serikali inaendelea nazo. 

No comments: