RAIS KIKWETE ATEUA KAMISHNA MKUU MPYA WA TRARais Jakaya Kikwete amemteua, Rished Bade kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Taarifa ya uteuzi huo imetolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni  Sefue.
Kwa mujibu wa Balozi Sefue uteuzi huo unaanza Mei 6, mwaka huu akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Harry Kitilya ambaye alistaafu   Desemba 14, 2013.
Kabla ya uteuzi huo, Bade alikuwa Naibu Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania na kukaimu nafasi ya Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania toka Kitilya alipostaafu.
Kamishna huyo mkuu mpya ana Shahada ya Kwanza ya Biashara na Menejimenti ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (1995); Shahada ya pili ya Biashara, Fedha na Benki ya Chuo Kikuu cha Sydney (1999), pia ni Mhasibu aliyethibitishwa na Bodi ya Wahasibu (CPA).
Wakati huo huo Rais Kikwete juzi amefanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Watu wa China,  Li Keqiang.
Rais alikutana na Waziri Mkuu huyo katika Hoteli ya Transcorp Hilton ya mjini Abuja nchini Nigeria ambako wote wawili wamefikia wakati wanashiriki Kongamano la Uchumi Duniani Afrika (World Economic Forum -Africa).
Taarifa ya Ikulu inasema kwamba viongozi hao wawili wamezungumzia, kimsingi, mambo yanayohusu uhusiano wa Tanzania na China.
Katika mkutano huo, Rais Kikwete amemuomba Li Keqiang kuisaidia Tanzania kuboresha mfumo wake wa kutunza na kuhifadhi nafaka kutokana na ongezeko kubwa la uzalishaji  wa nafaka, ambao unatokana na kukua kwa kilimo cha Tanzania. 
Waziri Mkuu Li Keqiang amekubali ombi hilo la Tanzania.
Rais Kikwete pia amemwomba Waziri Mkuu huyo wa China kusaidia kuhakikisha kuwa kazi ya ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo inaanza mapema iwezekanavyo, ombi ambalo Waziri Mkuu Li Keqiang pia amelikubali.
China ni moja ya wawekezaji wakuu katika uchumi wa Tanzania kwa kiasi cha dola za Marekani bilioni 2.5.

No comments: