RAIS KIKWETE AMLILIA MPIGAPICHA WA MLIMANI TV

Rais Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk Fenella Mukangara kufuatia kifo cha Mpigapicha wa Kituo cha Televisheni cha Mlimani, Maximilian John kilichotokea alfajiri ya Mei 24, mwaka huu.
“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Maximilian kilichotokana na maradhi ya moyo, sukari  na shinikizo la damu. Kifo hicho ni pigo na pengo kubwa kwa tasnia ya habari hapa nchini,” alisema  Rais Kikwete katika salamu hizo.
“Maximilian atakumbukwa kwa uchapakazi wake na uhodori katika kazi zake siku zote. Kifo ni maandiko ya Mwenyezi Mungu hivyo hatuna budi kumshukuru kwa yote.
“Nakutumia salamu zangu za dhati kuomboleza msiba huu. Aidha, kupitia kwako, naitumia familia ya Ndugu Maximilian, pole za dhati ya moyo wangu kwa kuondokewa na mzazi na mhimili wa familia. Aidha, salamu hizi ziwafikie pia wanahabari wote, wafanyakazi wenzake, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu.
“Nakuomba uwajulishe kuwa naelewa machungu yao katika kipindi hiki na nawaombea subira na uvumilivu. Ninaungana nao kumwomba Mwenyezi  Mungu, Mwingi wa Rehema, aiweke peponi roho ya marehemu. Amen,” amesema Rais katika salamu hizo. Maximilian ameacha mjane na watoto wanne.

No comments: