RAIS KIKWETE ABEBESHA WAKUU WA MIKOA MZIGO



Rais Jakaya Kikwete, amewaagiza wakuu wa mikoa kupunguza vifo vya watoto na akina mama vinavyotokana na uzazi katika mikoa yao, huku akiwahadharisha kwamba atafuatilia kwa karibu utendaji wao kuona namna wanavyoshughughulikia tatizo hilo.
Alionya kuwa hatakuwa na huruma na Mkuu wa Mkoa,  atakayeshindwa kuweka mikakati ya kupunguza tatizo hilo katika mkoa wake, na akawataka waachane na kisingizio cha ufinyu wa bajeti ambacho kimekuwa  kichaka cha viongozi wasiowajibika.
Akizundua mpango mkakati wa kuongeza kasi ya kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na  vya watoto wachanga na wale wa chini ya miaka mitano, Rais Kikwete alisema kuanzia sasa jambo la kwanza atakalofuatilia katika utendaji wa wakuu wa mikoa, ni namna wanavyoshiriki kupunguza vifo vya watoto na akina mama katika maeneo yao.
"Mimi sio kiongozi wa kusikiliza na kuamini ninayoambiwa, hili linanigusa kwa karibu… nawaambia nitafuatilia utendaji wenu kwa karibu, lengo nataka vifo vya watoto wachanga na wale wa chini ya miaka mitano pamoja mama wajawazito vinapungua," alisema Rais Kikwete.
Rais Kikwete alisema wakuu wa mikoa, wamekuwa hawafuatilii masuala ya afya hadi litokee tatizo la dharura la kipindupindu, wakati vifo vya watoto na akina mama wanaokufa kwa uzazi vinaongezeka hata kuliko wanaokufa kwa kipindupindu.
Aliwataka suala hilo iwe ajenda ya kisiasa katika ngazi zote za Serikali na akawaagiza wakuu hao wa mikoa, wanaporejea mikoani kwao wakasambaze maagizo hayo katika ngazi za chini yao, ili utekelezaji uanze mara moja.
"Wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya wanafikiri suala hili ni la waganga wakuu na watumishi wa afya, hata hawaulizi hali zikoje mikoani kwao, sasa lichukulieni hili kuwa la dharura...nikija huko jambo la kwanza kuuliza na kufuatilia ni suala hili," alisema Rais Kikwete.
Aliwataka wakuu hao wa mikoa kuweka mikakati ya kupunguza tatizo hilo na yeye akaahidi kuwa atalifuatilia binafsi utendaji wa kila Mkuu wa Mkoa, kupitia kadi maalum za kutolea taarifa za vifo vya watoto wachanga, watoto wa chini ya miaka mitano na akina mama wanaokufa kwa matatizo ya uzazi.
Alisema baadhi ya vifo vya watoto na wajawazito vinatokea kwa sababu ya uzembe wa watumishi wa afya, na akaeleza kuwa suala hilo linawezekana iwapo tu viongozi watatimiza wajibu wao kwa kufuatilia kwa karibu.
"Kipimo cha uwajibikaji wenu, itakuwa kupitia kadi hii," alisema Rais Kikwete na kuahidi kuwa atahitaji kupokea taarifa ya kila mkoa kila baada ya miezi minne, kuona namna wakuu wa mikoa na watendaji wao wanavyoshughulika na tatizo hilo.
Rais Kikwete alisema sekta ya afya kwa sasa haiko katika mpango wa matokeo makubwa sasa, ameagiza kitengo cha Rais cha kufuatilia utekelezaji wa Mfumo wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), waiweke sekta hiyo kwenye mpango huo.
Rais pia alitoa mwito kwa wajawazito, kuhakikisha wanapata chakula bora chenye lishe, ili kuongeza usalama wakati wanapoenda kujifungua. Alisema pia  familia zinatakiwa kuzingatia uzazi wa mpango, ili kuwalea watoto na kuwapa mahitaji yao ya msingi.
Awali akitoa tamko la wakuu wa mikoa, ambalo waliazimia juzi baada ya kufanyiwa semina, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk Christin Ishengoma, alisema wameazimia  kila mkoa uandae mpango mkakati wa kupunguza tatizo hilo ambao unatekelezeka na uwe shirikishi.
Alisema kuanzia sasa kila mkoa utawatambua wajawazito wote walioko katika maeneo yao na watoto wa chini ya miaka mitano, ili  kuwafuatilia kwa karibu na kuwapatia huduma za msingi zinazotakiwa.
Akitoa hali halisi ya vifo vya watoto na wajawazito wanaokufa kwa uzazi, Dk Neema Rusibamanyika, alisema akina mama 7,900 wanakufa kila mwaka kwa matatizo ya uzazi na vichanga 40,000 katika kila vizazi 100,000 pia hufariki.
Sababu za vifo vya watoto, alisema ni kuugua nimonia, magonjwa ya kuharisha na Malaria, wakati vifo vya wajawazito husababishwa na ukosefu wa vifaa tiba, upungugu wa watumishi, miundombinu mibovu na ucheleweshaji wa huduma.
Takwimu hizo zinaonesha kuwa asilimia 51 ya wajawazito ndio wanaojifungulia hospitalini, wakati asilimia 49 hujifungulia kwa wakunga wa jadi. 
Hali hiyo ni chini ya Malengo ya Millenia, yanataka ifikapo mwaka 2015 asilimia 80 ya wajawazito wawe wanajifungulia hospitalini.

No comments: