Waziri
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka amesema zoezi
la upangaji miji, haliwezi kufanikiwa, iwapo wanaohusika hukimbilia
mahakamani huku kesi zikichukua muda
mrefu kutolewa maamuzi.
Profesa
Tibaijuka alisema hayo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, wakati
akizungumza na watumishi wa wizara hiyo kwa lengo la kuwapatia nyenzo za
kujiboresha katika utendaji.
Kuhusu
mipango miji, alisema mchakato wa mahakama umekuwa ukiwakwamisha, jambo ambalo
husababisha utekelezaji wa mikakati yake ya upangaji miji kuchukua muda mrefu.
“Sio
kwamba tunaogopa wala kukosa nguvu katika kutekeleza zoezi la upangaji miji na
hata bomoabomoa...ni suala la kisheria ambapo wamenifunga kasi, kwani kila
anayehusika anakimbilia mahakamani,” alisema Profesa Tibaijuka.
Alitolea
mfano maeneo ya fukwe kuwa walioko huko, wamekwenda mahakamani, ambapo kwa hali hiyo kazi ya upangaji miji
haiwezi kufanikiwa, kwani hata mahakama pia hazina kasi na wakati mwingine
kuweza kusubiria hadi awamu nyingine ya uongozi.
Kuhusu migogoro ya wafugaji na wakulima, alisema
serikali ina mpango wa kurejesha baadhi ya ranchi zake kwa wafugaji ili kuacha
kutangatanga katika kutafuta malisho yaliyo bora kwa mifugo.
Wakati
huo huo, Rais Jakaya Kikwete amemteua Zakhia Meghji kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) huku Profesa Tibaijuka akiteua wajumbe saba wa
Bodi hiyo katika uteuzi ulioanza April mosi.
Aliwataja
wajumbe hao kuwa ni Charles Mafuru, Bedason Shallanda, Irene Isaka, Subira
Mchumo, Patrick Rutabanzibwa, Diotrephes Mmari na Samson Kassala.
Aidha
Profesa Tibaijuka amemteua Profesa Bavo Nyichomba kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya
Wakala wa Taifa wa Utafiti wa Nyumba na Vifaa vya Ujenzi (NHBRA) na wajumbe
watano Bodi hiyo ni Dk. Yususu Fundi, Moshi Zebedia, Dk. Nicolas Nyange, Hilda
Gion na Pius Tesha.
No comments:
Post a Comment