PROFESA LIPUMBA ANG'ANG'ANIA HOJA YA UKAWA

Pamoja na mwito wa Rais Jakaya Kikwete, wasomi na wanasiasa wakongwe na mashuhuri nchini, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba ameweka bayana kuwa chama chake na washirika wengine wanaounda kinachoitwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), hawatorejea kwenye Bunge Maalum la Katiba.
Kwamba, watakuwa tayari kufanya hivyo watakapojiridhisha kuwa kinachojadiliwa ni rasimu ya katiba inayotokana na mawazo ya wananchi ambayo roho yake ni sura ya sita inayoelezea muundo wa Muungano wa Serikali tatu.
Prof. Lipumba aliyasema hayo jana alipokuwa akifungua kikao cha kawaida cha siku tatu cha Baraza Kuu la Uongozi la CUF, kinachofanyika makao makuu ya chama hicho, Buguruni jijini Dar es Salaam.
Kauli ya Lipumba inakuja huku Rais Jakaya Kikwete, Spika wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta, viongozi wa dini, wasomi na wanasiasa wakongwe wakiwasihi `waumini’ wa Ukawa kuweka mbele maslahi ya taifa kwa kuamua kurudi bungeni kushiriki mchakato wa kutunga Katiba badala ya kususia na kuingia mtaani `kueneza’ chuki.
Katika kikao cha jana, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar alisema malengo makuu ya kikao chao ni pamoja na kufanya uteuzi wa mwisho kwa wagombea wa nafasi za ukatibu na uwenyeviti katika ngazi za Wilaya, pamoja na kuandaa na kupitisha Mkutano Mkuu wa Taifa.

No comments: