Vijana 700 wa Wilaya ya Kilombero
mkoani Morogoro, wamenufaika na mafunzo
ya ufundi wa stadi za awali za ajira za kuwawezesha kujiajiri wenyewe na
kuondokana kuwategemea wazazi wao na kuwaokoa katika wimbi la kukaa vijiweni.
Vijana hao wamenufaika na mafunzo
hayo chini ya ufadhili
wa Shirika la Plan International kwa kushirikiana na Serikali ya Canada
kupitia Shirika lake la Maendeleo (CIDA).
Mpango huo wa kuwawezesha vijana ni wa
miaka minne , ulianza mwaka 2011 na kutarajiwa kumalizika mwakani.
Meneja Miradi wa Plan Tawi la Ifakara,
Emmanuel Mmbaga , alisema hayo jana wakati akimkaribisha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya
hiyo, Azimina Mbilinyi, kwenye mahafali ya tatu ya wahitimu 150 wa
mafunzo ya ufundi wa stadi za awali za ajira kutoka vijiji kadhaa vya Tarafa ya Mang’ula, wilayani humo.
Kwa mujibu wa Meneja miradi huyo,
Shirika la Plan International limeona
umuhimu wa kuanzisha mpango huo hasa baada ya kuona changamoto mbalimbali
zinazowakabili vijana hapa Tanzania hususani
tatizo la ajira.
Hata hivyo alisema mpango huo
umezingatia usawa kwa asilimia 50 zilizo sawa kwa vijana wa kiume na wa kike
ambapo mafunzo hayo ni ya miezi minne katika fani ya udereva wa magari, upishi,
udereva wa magari madogo na pikipiki.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, katika hotuba
yake iliyosomwa na Ofisa Elimu wa
Sekondari wa wilaya hiyo, Jackson Mpankuly, aliwataka wazazi na jamii kuona umuhimu wa kuchangia mpango
huo.
Alisema kuchangia kwao katika mpango
huo, kutawahakikishia vijana nchini kutimiza malengo yao ya kujitengenezea
maisha na pia kuchangia namna ya
kukabiliwa na tatizo la ajira kwa vijana.
Katika mradi huo wa mafunzo, Plan
imeelekeza nguvu zake kwa vijana wa kata za Mang’ula, Mwaya, Kisawasawa,
Mchombe na Mngeta, hususani kwa vijana wanaoishi katika mazingira magumu.
No comments:
Post a Comment