PIGO TENA!! MWIGIZAJI MWINGINE WA FILAMU AFARIKI DUNIA

Habari zilizotufikia hivi punde zinasema mwigizaji filamu wa Swahilihood, Rachel Haule amefariki dunia asubuhi hii kutokana na matatizo ya uzazi. 
Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari, zinasema Rachel alikwenda hospitalini jana kwa ajili ya kujifungua na kwamba ndipo ikagundulika na matatizo yaliyosababisha oparesheni ambayo haikufanikiwa na hivyo kulazimika kuhamishiwa chumba cha wagonjwa mahututi.
 Chanzo hicho licha ya kutotaja jina la hospitali hiyo, kiliendelea kusema kwamba baada ya oparesheni hiyo ikagundulika mtoto aliyekuwa tumboni alikwishafariki hiyo jana licha ya juhudi kubwa na madaktari kujaribu kuokoa maisha yake.

Baada ya kushindwa kwa mtoto, kipaumbele cha pili kikawa kuokoa maisha ya mama (Rachel) ambaye pia haikuweza kufanikiwa na kufariki dunia masaa kadhaa baadaye (leo asubuhi).
Rachel enzi za uhai wake alijizolea umaarufu mkubwa kupitia filamu kadhaa alizoshirikishwa na Jennifer Kyaka 'Odama' ambaye ameelezwa kuwa rafiki yake mkubwa.
Moja ya filamu zilizomtangaza sana Rachel na kuthibitisha kipaji alichonacho ni ile ya 'Dilemma'.
Hili ni pigo la pili kwa tasnia ya filamu hapa nchini, kwani limekuja katika kipindi kisichozidi wiki mbili baada ya tasnia hii kuondokewa na mwigizaji na mwongozaji filamu maarufu, Adam Kuambiana.
Mungu aiweke roho ya marehemu Rachel mahali pema peponi, Amina.

No comments: