NGOMA ZA KHANGA MOKO, KIGODORO SASA MARUFUKU



Ngoma za kigodoro, khanga moko  na nyingine ambazo  huchezwa usiku katika maeneo kadhaa jijini Dar es Salaam, zimepigwa marufuku na polisi kwa kile kilichoelezwa zimegeuzwa kuwa sehemu ya uhalifu.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, alitaja ngoma nyingine zinazochezwa usiku na kukesha  na zinazotajwa kutumiwa na baadhi ya watu, hususani vijana  kwa uhalifu ni mnanda, mchiriku na baikoko.
Kwa mujibu wa Kova, polisi imebaini vijana wanaojihusisha na vikundi vya uhalifu vilivyojiita majina ya Mbwa Mwitu au Panya Road, hupenda kushiriki katika ngoma za mnanda, mchiriku, kigodoro na nyingine za aina hiyo, ambazo kwa kawaida huchezwa hadi usiku wa manane.
Kova aliwaambia waandishi wa habari ofisini kwake kwamba, "Imegundulika pia vijana hawa wanatumia dawa za kulevya aina ya bangi na wengine hujichoma sindano na kuwafanya iwe rahisi kujihusisha na matukio ya uhalifu.”
Alisema mara nyingi vijana hao, wakitoka katika ngoma hizo, hujikusanya na kufanya matukio ya uporaji kwa mtu wanayekutana naye na pia huvunja nyumba na maduka na kupora.
Kutokana na hali hiyo, Kova alisema kwa sasa wanajaribu kuwasiliana na Maofisa  Utamaduni katika wilaya zote za Dar es Salaam; Ilala, Kinondoni na Temeke,  kuhakikisha hawatoi vibali vya ngoma za usiku zisizo na tija.
Wakati huo huo,  Kova alisema wamekamata vijana 149 wanaotuhumiwa kujihusisha na vikundi vya uhalifu,  vilivyojiita majina ya  Mbwa Mwitu au Panya Road.
"Kuna kikosi maalumu kilichoundwa ambacho lengo lake ni kuhakikisha kuwa vikundi hivyo haviibuki tena na vinatokomezwa kabisa  kwa kuwakamata wale wote wanaojihusisha na vitendo vya kuvamia kwa makundi wananchi ambao hawana ahatia," alisema Kova.
Alisema vijana hao wamekamatwa katika msako mkali wa nyumba kwa nyumba, uliofanyika ndani ya saa 24 kwa lengo la kukabili vikundi vya vijana hao wasio na ajira, waliojiunga kufanya uhalifu.
Kamanda alisema kati ya waliokamatwa, yumo kijana mwenye umri wa miaka 20 mkazi wa Kigogo, ambaye waligundua ndiye kiongozi. Alisema kijana huyo (jina tunalihifadhi), alikiri kuongoza kundi la watu zaidi ya 15, ambao baadhi yao wamekamatwa.
Kova alitaja baadhi ya majina ya waliokamatwa. Hata hivyo, alisema "zipo taarifa za kuwa baadhi ya wazazi wasio waaminifu wamewasafirisha watoto wao wahalifu katika makundi haya kwenda mikoani ili kukwepa wasinaswe na msako huu, lakini tunawaambia tuna mtandao mkubwa na tutawakamata," alisema.

No comments: