NDEGE ZA ATC KARIBU KUANZA KUNG'ARA TENA HEWANI



Shirika la Ndege Tanzania (ATC), lipo karibu kuanza kung’ara hewani baada ya mwekezaji kutoka Oman, kuwa tayari kuwekeza kwenye shirika hilo na sasa anasubiri Serikali kukamilisha taratibu zake.
Miongoni mwa taratibu zinazosubiriwa ni kwa Serikali kulipa madeni makubwa ambayo ATC ilikuwa inadaiwa, ili kuweka mizania sawa ya vitabu vya hesabu za fedha.
Mwenyekiti na Rais wa kampuni za Al Hayat Development and Investment LLC za Oman, Sheikh Salim Bin Abdullah Al Harthy, alisema wana dhamira ya dhati ya kuwekeza hapa nchini na hasa katika ATC.
“Tunatarajia kuwekeza kwenye maeneo tofauti katika sekta za mafuta na uendelezaji wa maeneo ya fukwe, lakini lengo letu kuu ni kuwekeza ATC,” alisema Sheikh Salim na kuwa awamu ya kwanza watatumia Sh, bilioni 160.
“Mpango wetu ni kujenga kituo cha mafunzo ya masuala ya ndege, ofisi nzuri kwa ajili ya ATC, kununua ndege na kufanya shughuli nyingine za maendeleo. Tunatarajia kufanya haya katika kipindi kifupi kijacho," alisema.
Alifafanua kuwa kuna wakati Kampuni ya Al Hayat ilikaa kimya kuhusu uwekezaji huo na ilifanya hivyo ili kutoa nafasi kwa Serikali kukamilisha taratibu zake ikiwemo kupitia makubaliano yaliyofikiwa kati ya kampuni hiyo na ATC.
Alisema watendaji wa Kampuni ya Al Hayat wamekuwa wakitembelea Tanzania mara kwa mara, kufuatilia suala zima katika uwekezaji kwenye ATC.
Shekhe Salim alisema ni kutokana na hali hiyo, ndiyo maana hata ule mpango wa kununua ndege aina ya Bombadier, Air Bus na Embraer ulisimama kidogo kwa kuwa mkataba rasmi wa uwekezaji bado haujafikiwa na kutiwa saini.
Alisema safari hii wamekuja tena kuitikia mwito wa ATC ili kuendeleza makubaliano yaliyofikiwa na kuwa taratibu zikikamilika watatia saini mkataba na kuanza uwekezaji.

No comments: