MZINDAKAYA AKERWA KIKWETE KUFITINISHWA NA KAGAME

Mwanasiasa mkongwe nchini, Dk Chrisant Mzindakaya amekemea baadhi ya vyombo vya habari nchini, kuacha kuandika habari za uchochezi kwamba kutohudhuria kwa Rais Paul Kagame wa Rwanda kwenye sherehe za Maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano, kunaashiria kuwa bado kuna tofauti za kisiasa kati ya nchi mbili hizo.
Alisema katika sherehe hizo, zilizofanyika mapema wiki iliyopita, Rais Kagame aliwakilishwa na Waziri Mkuu wake, Pierre Habumuremyi na kuonesha kwamba uhusiano kati ya nchi hizo bado ni mzuri na imara.
“Rwanda iliwakilishwa na ujumbe wa hali ya juu, hivyo kutofika kwa Rais Kagame isiwe nongwa  kwamba kuna tofauti za kisiasa kati ya Tanzania na Rwanda,” alisisitiza Dk Mzindakaya na kuongeza kuwa wanaoendeleza hoja hizo ni wachochezi.
Alifafanua kuwa Rais Jakaya Kikwete katika sherehe za Maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano,  aliwaambia umati wa wageni waliohudhuria sherehe hizo kuwa Tanzania haina ugomvi na Rwanda na kwamba zinaishi kwa kushirikiana kwa udugu na upendo.
Alikanusha taarifa za baadhi ya vyombo vya habari, kwamba Rais Kikwete aliwatisha wananchi kwa kuonesha vifaa vingi vya kivita na mazoezi ya kijeshi katika maadhimisho hayo, kuonesha kwamba Jeshi linaweza kuchukua nchi, iwapo muafaka wa muundo  wa serikali hautapatikana, kuwa huo ni ufinyu wa busara.
Alifafanua kuwa, vifaa mbalimbali vya kivita na mazoezi ya kijeshi, vilivyooneshwa katika sherehe hizo, ililenga kuonesha mafanikio ya miaka 50 ya Muungano imara, yaliyopatikana tangu Muungano huo ulipozaliwa Aprili 26, 1964 na kuongeza kuwa wachochezi hao hawaitakii mema na mafanikio Tanzania.
Alimpongeza Rais Kikwete, Rais wa Zanzibar na Baraza la Mapinduzi, Dk Mohamed Shein na viongozi mbalimbali wa Serikali waliosimamia na kuhakikisha kuwa sherehe hizo za Muungano zinafana.
Aliwaomba Watanzania kuendelea kuelekeza akili zao katika kuimarisha Muungano, hasa wa serikali mbili.

No comments: