MWILI WA MENEJA BIASHARA EWURA KUAGWA LEO



Meneja Biashara ya Mafuta wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), Julius Gashaza (pichani kulia) aliyefariki dunia juzi, anatarajiwa kuagwa leo nyumbani kwake Yombo Vituka, Dar es Salaam.
Shughuli za kuagwa kwa mwili huo zinatarajiwa kuanza saa 5 asubuhi kabla ya kusafirishwa kwenda nyumbani kwao wilayani Ngara.
Mmoja wa wanafamilia ambaye hakutaka jina lake kuandikwa akizungumza kwa majonzi na mwandishi jana, alisema shughuli za kuagwa mwili huo zitafanyika nyumbani hapo zikiambatana na misa ya kumuombea.
Awali ndugu huyo ambaye alikataa kutajwa gazetini, alisema kuwa kifo cha Gashaza ni pigo kubwa kwa familia hiyo, lakini hawana cha kufanya zaidi ya kuachia Polisi kufanya kazi yao.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Felix Ngamlagosi, Gashaza aliajiriwa na mamlaka hiyo 2006 akiwa Mkaguzi Mkuu wa Mafuta ya Petroli.
Mwaka 2013 Gashaza aliteuliwa kuitumikia Mamlaka hiyo katika cheo cha Meneja wa Biashara kwenye Idara hiyo ya Petroli.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa mnamo Mei 15, mwaka huu Gashaza alisafiri kwenda Dodoma kwa usafiri wa ndege akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Ewura kwenye kikao cha Kamati ya Bunge ya Bajeti.
"Baada ya kikao hicho, alirejea jijini Dar es Salaam Jumamosi   Mei 17, 2014 saa tatu usiku. Asubuhi ya siku iliyofuata, tarehe 18 Mei 2014, uongozi wa Ewura ulipokea taarifa za kushtua toka kwa familia yake kwamba Gashaza amefariki dunia," ilieleza taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa mamlaka hiyo inaendelea kuratibu taratibu za mazishi, ambapo utasafirishwa kwenda Wilaya ya Ngara, nyumbani kwao marehemu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Engelbert Kiondo,  alisema Gashaza alikutwa amejinyonga kwenye nyumba ya kulala wageni  ya Mwangaza Lodge kwa kutumia tai aliyoiunganisha na waya wa pazia na kuitundika kwenye nondo za dirisha la chumba namba 113.
Kamanda Kiondo alisema chanzo cha kifo chake hakijafahamika lakini inasadikiwa kuwa siku ya Mei 17, aliwaeleza ndugu zake kuwa ana matatizo ya kiofisi ambayo hata hivyo hakuyaweka wazi.

No comments: