MWANDISHI WA HABARILEO ASHINDA TUZO YA TANAPA

Mwandishi wa HabariLeo, Iringa, Frank Leonard ametwaa tuzo ya kuandika vizuri habari za utalii wa ndani.
Frank amekuwa mshindi wa pili kwa upande wa magazeti.
Kwa ushindi huo, Frank alizawadiwa Sh milioni 1.5 , cheti na ziara katika hifadhi nchini. Tuzo hizo zilitolewa  na Hifadhi ya Taifa (TANAPA).
Mshindi wa kwanza alikuwa Gerald Kitabu kutoka The Guardian Limited aliyejinyakulia Sh milioni 2, ngao, cheti na atapata safari ya kwenda nje  ya nchi kujifunza utalii na mshindi wa tatu alikuwa Jackson Kalindimya kutoka Nipashe ambaye alikabidhiwa Sh milioni na cheti.
Washindi  kwa kipengele cha utalii wa ndani kwa upande wa radio, mshindi wa tatu  hakupatikana kutokana na washiriki kutokidhi vigezo vilivyokuwa vikitolewa na majaji na badala yake Humphrey Mgonja kutoka Radio Five aliibuka mshindi wa pili na wa kwanza ambapo alikabidhiwa Sh 3.5m, cheti na atapata ziara ya mafunzo kutoka katika hifadhi mbili za hapa nchini na safari ya kwenda nje ya nchi kujifunza.
Waliobuka washindi kwa kipengele cha utalii wa ndani kwa upande wa televisheni ni Kakuru Msimu kutoka Star Tv aliyekuwa mshindi wa tatu, Kasiasi Mdame alitangazwa kuwa mshindi wa pili halikadhalika katika kipengele hiki mshindi wa kwanza hakupatikana kutokana na washiriki kutokidhi vigezo vya majaji.
Walioibuka ushindi kwa habari za uhifadhi kwa upande wa magazeti, alikuwa ni mwandishi pekee wa kike Salome Kitomari aliyeibuka mshindi wa tatu na kukabidhiwa kitita cha shilingi milioni moja na cheti, washindi wa pili na wa kwanza hawakupatikana kutokana na washiriki kutokidhi vigezo vya majaji.
Walioibuka washindi kwa upande wa televisheni kwa kuandika habari za uhifadhi, Vedasto Msungu kutoka ITV aliibuka kidedea kwa kuwa mshindi wa kwanza, ambapo alikabidhiwa kitita cha Sh milioni 2, ngao, cheti na kama walivyo washindi wengine atapata ziara ya mafunzo kwa nchi za Sadc, mshindi wa pili alikuwa ni Raymond Nyamwihura kutoka Star Tv ambapo alikabidhiwa Sh milioni 1.5 na cheti na atapata ziara ya mafunzo kutoka katika hifadhi za taifa za hapa nchini na mshindi wa tatu hakuweza kupatikana.
Awali akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Tanapa, Ali Kijazi alisema Tanapa iliamua kuanzisha tuzo kwa waandishi wa habari nchini, kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kuandika na kutangaza kwa kina habari za utalii wa ndani na uhifadhi.
Alisema TANAPA imeendelea kuboresha mashindano hayo ya kuwania tuzo hizo, ambapo kwa mwaka huu jumla ya kazi 114 ziliwasilishwa na waandishi kwa mwaka huu tofauti na kazi 74 zilizowasilishwa mwaka jana, ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 235.

No comments: