MVUA ZASABABISHA MFUMUKO WA BEI KUJICHEKECHA



Mvua zinazoendelea kunyesha sehemu mbalimbali nchini, zimesababisha mfumuko wa bei wa taifa kwa mwezi Aprili kuongezeka hadi kufikia asilimia 6.3 kutoka asilimia 6.1.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kuwepo kwa mfumuko huo wa bei kumetokana na fahirisi ya bei ya bidhaa mbalimbali kuongezeka hadi 150 mwezi Aprili mwaka huu kutoka 141.59 mwezi Aprili mwaka 2013.
Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii wa NBS Ephraim Kwesigabo, alisema jana kuwa mfumuko wa bei  wa mwezi Aprili umeongezeka kutokana na baadhi ya bidhaa za vyakula kuongezeka bei pamoja na bidhaa zisizo za chakula hasa mkaa.
Mchele unaelezwa kuwa bei yake imepanda kwa asilimia 3.5, mahindi asilimia 2.5, unga wa muhogo asilimia 4.8, kuku wa kienyeji asilimia 1.3, dagaa asilimia 6.0, samaki wakavu asilimia 7.8, matunda kwa asilimia 1.4 na karanga asilimia 2.6 .
Mkaa ambao unaangukia katika kundi la bidhaa zisizo za chakula umechangia kuongezeka kwa mfumuko wa bei kwa asilimia 4.3, huduma za matibabu asilimia 3.0, dizeli asilimia 4.4 na gharama ya kusaga nafaka nayo iliongezeka kwa asilimia 6.6.
Kwesigabo alisema mfumuko wa mwezi Aprili mwaka huu ambao unapimwa kwa kipimo cha mwezi umeongezeka kwa asilimia 0.7 ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 0.6 iliyokuwa mwezi Machi mwaka huu.
Alisema mfumuko kwa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi umeongezeka hadi asilimia 7.8 mwezi Aprili kutoka asilimia 7.2 ya mwezi Machi mwaka huu.
Alipoulizwa sababu ya kuongezeka kwa bei hizo, Kwesigabo alisema "Licha ya kuwa hatujafanya utafiti lakini mvua zinazoendelea kunyesha sehemu mbalimbali nchini zimechangia kuwepo kwa mfumuko wa bei."
Alisema gharama za usafirishaji wa bidhaa kutoka mashambani kwenda kwenye miji mikuu ya mikoa imeongezeka hali ambayo imechangia kuwepo kwa ongezeko hilo.

No comments: