MTAMBO WA MAJI WA RUVU JUU KUPANULIWASerikali  imeanza kupanua mtambo wa maji wa Ruvu Juu ili  kuongeza uzalishaji maji kutoka lita milioni 82 hadi milioni 196 kwa siku, imeelezwa.
Pia imeelezwa kuwa ukosefu wa malighafi, umesababisha matengenezo ya  mtambo huo uliopo Mlandizi Wilaya ya Kibaha, kuchelewa.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe wakati akitoa ufafanuzi kuhusu matatizo ya uzalishaji wa maji katika mtambo huo, kutokana na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika kuomba mwongozo bungeni.
Mnyika alitaka Serikali itoe kauli, kueleza matatizo yanayoukabili mtambo wa kuzalisha na kutibu maji kwa ajili ya Jiji la Dar es Salaam na katika Mkoa wa Pwani.
Profesa Maghembe alisema kuwa gharama za mradi wa upanuzi wa mtambo huo ni dola za Marekani milioni 39.7,  ambapo mkandarasi ameshaanza kazi Februari mwaka huu na atakamilisha Agosti 14, mwakani.
Alisema uwezo wa mtambo huo ni kuzalisha maji lita milioni 82 kwa siku na unaendeshwa kwa kutumia seti tatu za pampu katika shughuli za uzalishaji maji.
Alisema kwa nyakati tofauti, matengenezo yamechukua muda mrefu, kutokana na kutokupatikana  kwa wakati malighafi zinazohitajika.
Alisema wizara katika kukabiliana na matukio hayo, imechukua hatua za kuchonga vipuri na vifaa vya pampu katika karakana zilizopo nchini kwa kutumia wataalam wa jeshi, kuagiza vipuri nje ya nchi na kutoa matangazo kwa wananchi kuhusu upungufu wa maji pale uzalishaji unaopungua au kusimama.
Aliongeza kuwa pamoja na kuchukua hatua za dharura, vifaa na vipuri vya ziada vimeagizwa kutoka nje ya nchi na vingine kuchongwa katika karakana za ndani na kuvihifadhi kwa ajili ya dharura.
Pia, alisema mpaka sasa zipo seti mbili za pampu kwa ajili ya dharura. Aidha,  Mtambo wa maji Mtoni unafanyiwa ukarabati na Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA), wameagiza pampu mbili mpya kwa ajili ya kuchotea maji ghafi.
"Pampu hizi zitawasili Agosti mwaka huu. Mkandarasi amekamilisha tathmini ya ukarabati unaohitajika ili mtambo ufanye kazi vizuri katika kipindi chote cha mpito cha miezi 18 wakati mtambo mpya unajengwa," alisema.
Aidha, alisema Serikali inaendelea kudhibiti wizi mkubwa wa maji, unaofanyika katika Jiji la Dar es Salaam katika maeneo ya Kinondoni, Mwananyamala, Kigogo, Mabibo, Magomeni, Tegeta, Kiluvya, Kibamba, Mbezi na Kimara.
Alisema jumla ya watuhumiwa wa wizi wa maji 162, wamekamatwa na kufikishwa mahakamani hadi sasa.
Watuhumiwa 23 walipatikana na hatia ambapo 19 waliamriwa kulipa faini ya kati ya Sh 200,000 na Sh 2,316,400 na watuhumiwa wanne walifungwa.
Aliongeza kuwa kumekuwa na matukio mengi na ya kufululiza ya kuathiri uzalishaji wa maji katika mtambo wa kusafishia maji wa Ruvu Juu.
Matatizo hayo yanahusu kuharibika kwa pampu, umeme kukatika mara kwa mara na kupasuka kwa mabomba.
Alisema Wizara imeunda Kamati maalumu, ambayo imeanza kufanya tathmini ya kina, kujua chanzo cha matukio hayo.
Alisema kamati hiyo itafanya uchunguzi, kubaini kama matatizo hayo yanatokana na mifumo ya kiufundi, kiuendeshaji au makosa ya kibinadamu.
Kamati inatarajiwa kutoa taarifa yake katika kipindi cha mwezi mmoja na hatua zitaendelea kuchukuliwa ili kuhakikisha mtambo unarudi katika hali yake ya kawaida.

No comments: