Mbunge wa
Ubungo, John Mnyika amemshitaki Mwenyekiti Mtendaji wa Simon Group inayoendesha
Kampuni ya Usafiri Dar es Salaam (UDA), Robert Kisena kwa Spika wa Bunge, Anne
Makinda, kutokana na kudai wabunge wa Dar
es Salaam
wamehongwa.
Katika mkutano
wake na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki, Kisena alidai kushangazwa na
upotoshwaji unaofanywa na Mnyika juu ya uhalali wa umiliki wa hisa za shirika
hilo.
Kisena alikwenda
mbali zaidi na kudai mbunge huyo anatumiwa na mfanyabiashara mmoja aliyedai
kuwa tangu 2001 amekuwa akiendesha kampeni chafu ya kuichafua Simon Group
Limited.
Lakini jana
bungeni, Mnyika akitumia Kanuni za Bunge, alisema Kisena amekiuka kanuni
hizo kwa kuwatuhumu wabunge kuwa wamehongwa, ilhali Serikali ndiyo iliyoweka
bayana umiliki wa Uda.
Kwa mujibu wa
Mnyika, wiki iliyopita katika kujibu swali la Mbunge wa Kawe, Halima Mdee
(Chadema), Serikali ilisema hisa za Uda zinamilikiwa kwa asilimia 100, tofauti
na madai ya Kisena aliyedai wanamiliki asilimia 76 na zilizobaki zinamilikiwa
na Serikali.
Katika jibu lake
kwa swali hilo, Naibu Waziri wa Fedha, Adam Malima, alisema Serikali inamiliki
asilimia 100 katika Uda kwa maana asilimia 51 zinamilikiwa na Halmashauri ya
Jiji na asilimia 49 za Msajili wa Hazina.
Aidha, Malima
alikiri kuwapo kwa utata kuhusu kwa mazingira ya uuzwaji wa shirika hilo kutoka
pande zote mbili za umiliki yaani Halmashauri ya Jiji na Serikali.
Mnyika alisema
Kisena ameingilia uhuru wa majadiliano bungeni ambao kwa mujibu wa Kanuni na
Sheria za nchi, kwamba hautahojiwa nje ya Bunge, hivyo akataka apelekwe katika
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kinga, Haki
na Madaraka ya Bunge.
“Kwa hiyo,
Mheshimiwa Spika, nataka suala hilo lifikishwe mbele ya Kamati ya Kinga, Hadhi
na Madaraka ya Bunge kwani amekiuka haki ya majadiliano bungeni,” alisema
Mnyika.
Katika hoja yake,
Mnyika alirejea habari zilizoandikwa na gazeti hili na la Uhuru, katika matoleo
yao ya juzi.
Kutokana na hilo,
Spika Makinda ameigiza Kamati ya Kinga, Hadhi na Madaraka ya Bunge, ilifanyie
kazi na kumpelekea majibu kwake kwa hatua za utekelezaji.
Aidha, Makinda
alikataa mwongozo uliokuwa ukiomba
kuhusu madai ya kuwapo kwa vyeti feki vya taaluma vikiwahusisha wabunge na
mawaziri kutokana na kitabu kimoja kilichoandikwa nchini.
No comments:
Post a Comment