MKURUGENZI MTENDAJI TANESCO NA MKEWE KIZIMBANI KWA UFISADIAliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), William Mhando, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na mashitaka ya kutumia vibaya madaraka kwa kutoa zabuni ya usambazaji wa vifaa kwa kampuni inayomilikiwa na mkewe.
Mbali na Mhando, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni mkewe Eva Mhando, ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Santa Clara Supplies. Wengine ni Wahasibu Wafawidhi wa Tanesco, France Mchalange na Sophia Misidai pamoja na Ofisa Ugavi, Naftali Kisinga.
Washitakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka na Wakili kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leornald Swai mbele ya Hakimu Mkazi, Frank Moshi.
Kwa mujibu wa mashitaka yaliyosomwa mahakamani, Mhando alitumia vibaya madaraka yake kwa kutoa zabuni ya kusambaza vifaa vya ofisi vyenye thamani ya Sh 884,550,000 kwa kampuni inayomilikiwa na mkewe.
Wakili Swai alidai kati ya Aprili Mosi na Desemba 31, mwaka 2011 katika Makao Makuu ya Tanesco, Mhando alitumia vibaya madaraka kwa kushindwa kuelezea ana maslahi na kampuni ya Santa Clara ambayo mkurugenzi wake ni mkewe Eva na mtoto
wake, hivyo kuiwezesha kupata mkataba kusambaza vifaa vya ofisi wenye thamani ya Sh 884,550,000 na kuipa faida ya Sh 31,747,000.
Katika mashitaka yanayomkabili Eva, Swai alidai kati ya Januari 6 na Julai 30, mwaka 2011, sehemu isiyofahamika Dar es Salaam, alighushi ripoti ya ukaguzi wa fedha ya Kampuni ya Santa Clara kwa mwaka 2007/2008, kuonesha kuwa Finx Capital House ilifanyia ukaguzi kampuni hiyo jambo ambalo si kweli.
Aidha inadaiwa  Agosti 9, mwaka 2011, kwa njia ya udanganyifu, mke huyo wa Mhando alighushi nyaraka za uhamishaji wa hisa kuonesha kwamba amehamisha hisa 200 ambazo kila moja ina thamani ya Sh 10,000 kutoka kwa kampuni yake kwenda kwa Eveta John Shing'oma, jambo ambalo si kweli.
Swai aliendelea kudai kuwa, Agosti 5, 2011, katika Makao Makuu ya Tanesco, huku akijua ni kwa nia ya udanganyifu, aliwasilisha kwa Katibu wa Bodi ya Zabuni ya shirika hilo, ripoti ya ukaguzi wa fedha wa kampuni yake kuonesha imeandaliwa na Finx Capital House.
Pia anadaiwa alijipatia Sh  31,747,000 kwa njia ya udanganyifu. Anadaiwa kujipatia fedha hizo, kwa kusambaza vifaa vya ofisi, baada ya kuwasilisha nyaraka za kughushi.
Nyaraka hizo zinadaiwa kuwa ni ripoti ya ukaguzi wa fedha  na orodha ya mikataba ya miaka miwili. Anadaiwa kuwasilisha nyaraka hizo kwa Katibu wa Bodi ya Zabuni ya shirika hilo,  kuonesha kwamba kampuni yake ilistahili kupewa zabuni kusambaza mashine ya kutoa nakala za karatasi na kompyuta kwa mwaka 2011.   
Katika mashitaka mengine, Mchalange, Sophia na Kisinga wanadaiwa Oktoba 17, mwaka 2011  katika makao makuu ya Tanesco, wakiwa wajumbe wa Kamati ya Tathimini ya zabuni ya usambazaji wa vifaa vya ofisi kwa mwaka huo, walitoa taarifa za uongo kuonesha Santa Clara, imekidhi vigezo vya kupatiwa zabuni ya kusambaza vifaa hivyo, huku ikiwa ni kinyume cha sheria.
Washitakiwa hao walikana mashitaka na Wakili Swai alidai upelelezi wa shauri hilo umekamilika.
Hakimu Mushi alisema washitakiwa watapata dhamana endapo watakuwa na wadhamini wawili wa kuaminika ambao watasaini hati ya Sh milioni nane kila mmoja. Aidha washitakiwa hawatakiwi kutoka nje ya mkoa wa Dar es Salaam, bila ya kibali cha mahakama.
Wote wako nje kwa dhamana baada ya kukamilisha masharti hayo ya udhamini.

No comments: