MKURUGENZI ALALAMIKIWA KWA MIKOPO YA WANAWAKE NA VIJANA

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdallah Bulembo ameilalamikia Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea, kwa tuhuma ya kushindwa  kutoa Sh 130,000,000 za mikopo ya kinamama na vijana.
Alisema hayo juzi  alipozungumza na viongozi wa ngazi mbalimbali wa chama hicho kwenye Ukumbi wa Chuo cha Ualimu Nachingwea mjini hapa.
Bulembo ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, alisema kamwe hawezi kuifumbia macho kadhia hiyo, endapo hatapewa taarifa za haraka kuwa fedha hizo zimepelekwa kwa walengwa.
“Sheria inasema Mkurugenzi (Mtendaji) wa Halmashauri ya Wilaya asiyetoa fedha hizo, anakuwa hana sifa ya kuendelea na wadhifa huo”, alisema huku akishangiliwa na viongozi hao, ambapo takribani wote walikiri kutofahamu kwamba kuna fungu hilo.
Alisema fedha hizo huwa hazipo kwenye bajeti ya halmashauri wala hazitoki serikalini, badala yake huwa zinatokana na asilimia 10 ya makusanyo ya ndani.
“Watu wanataka kero zao zimalizwe”, alisema huku akiwalaumu pia madiwani wa halmashauri hiyo wanaotokana na CCM, kwa kutochukua hatua zozote wakati wanakutana mara nyingi kwenye vikao vya baraza na vya kamati zake na hasa ya fedha.
Alipowapa nafasi wananchi ya kuuliza maswali kwa wakuu hao wa idara na kueleza kero walizonazo, baadhi ya tuhuma zilizotolewa ni ukosefu wa dawa katika hospitali ya wilaya, lakini kwenye maduka ya dawa zikipatikana wakati wote.
Hata hivyo, kero hiyo ilijibiwa na Kaimu Mkuu wa Idara ya Afya kwamba inatokana na urasimu uliopo katika Bohari ya Dawa ya Serikali.
Katika shughuli za kisiasa, Bulembo alipokea wanachama wapya 1,185 wa CCM, 527 wa Umoja wa Vijana (UVCCM), 471 wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) na 550 wa Jumuia ya Wazazi.
Kati ya hao, wengine wamevihama vyama vya upinzani hususan Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Civic United Front (CUF).

No comments: