MIGODI 18 YA TANZANITE KUFUTIWA LESENI


Migodi 18 ya madini aina ya tanzanite yaliyopo Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara inafutiwa  leseni ya uchimbaji baada ya wamiliki wa migodi hiyo kukiuka sheria ya madini. 
Migodi inayokumbwa na sakata hilo ni ile iliyopo katika kitalu B na D na yote iko mpakani mwa kitalu C kinachomilikiwa na kampuni ya TanzaniteOne. 
Akizungumza na mwandishi ofisi kwake, Kamishina Msaidizi wa madini Kanda ya Kaskazini, Alex Magayane alisema kuwa migodi hiyo imekiuka sheria iliyowekwa na Wizara ya Nishati na Madini na kupitishwa na bunge inayowaelekeza wachimbaji kuchimba madini kwa wima na sio vinginevyo. 
Magayane alisema kuchimba madini kwa mserereko na kuingia kuchimba madini katika kitalu C ni ukiukwaji mkubwa wa sheria hivyo ni lazima sheria ichukue mkondo wake bila ya kuoneana haya. 
Kamishina huyo wa madini aliendelea kusema kuwa  mara kwa mara ofisi yake imekuwa ikisisitiza uwajibikaji wa kufuata sheria na iwapo mmiliki hatafuata sheria ofisi yake haitavumilia hilo.

No comments: