MGOMO WA WAFANYAKAZI WA STRABAG WAMALIZIKA



Wafanyakazi wa Kampuni ya Strabag inayojenga barabara za kasi jijini Dar es Salaam,  wamerejea kazini baada ya mgomo wa siku saba.
Hayo yamethibitishwa na Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Migodi, Nishati, Ujenzi na Kazi nyinginezo (TAMICO), Abdulah Rukusa wakati akifanya mahojiano na gazeti hili jijini Dar es Salaam.
Alisema mgomo wa wafanyakazi hao, haukuwa chini ya chama hicho, ila baadhi ya wafanyakazi waliamua kufanya mgomo  baada ya kutokea vipeperushi vyenye kuashiria  suala la ubaguzi.
Aliongeza kuwa wafanyakazi hao, ambao ni Watanzania walilalamika kuwa kuna ubaguzi unaofanywa na kampuni hiyo kwa wafanyakazi huku wafanyakazi kutoka Kenya, Wahindi na Wazungu  wakipewa kipaumbele kuliko wao.
Alisema, wafanyakazi hao walidai wanabaguliwa na kampuni na hawapatiwi zana za kazi, kama  wengine na hata zikitolewa, wanapewa kwa ubaguzi.
 Pia,  walikuwa wakidai posho, ambazo kwa madai zinatolewa kibaguzi, vibarua hawapewi ila wenzao wa nje wanapewa na waliamua kupeleka madai yao kwenye Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) na kwamba posho zilisitishwa tangu Oktoba mwaka jana.
“Madai hayo yalipelekwa mahakamani na posho zilisitishwa mpaka Mei 15, mwaka huu kesi itakaposikilizwa tena,” alisema Rukusa.
Aidha, alisema baada ya RAS, DART na Strabag kukaa waliona madai ya wafanyakazi yana uzito na waliwasihi wafanyakazi kurejea kazini na waendelee kusubiri.
Baada ya wafanyakazi kurejea kazini, kampuni imewateua wafanyakazi 20 kwa ajili ya kwenda kusikiliza kesi hiyo.
“Kuna baadhi walikuwa wanapinga kurejea kazini, lakini walirudi,  ila kwa sasa kazi inaendelea kama kawaida,” aliongeza.
 Rukusa alisema watahakikisha wafanyakazi wanapewa zana za kazi bila ubaguzi na madai yao yanashughulikiwa kwa wakati ili kuepusha migogoro, ambayo inakwamisha ujenzi.

No comments: