Jopo
la marais wa zamani wanaoshughulikia mgogoro wa Ziwa Nyasa baina ya Tanzania na
Malawi, linasaubiri kumalizika kwa uchaguzi Mkuu wa Malawi unaotarajia
kufanyika Jumanne ijayo, ili kuingia katika awamu ya pili ya mazungumzo ya
kumaliza mgogoro huo.
Hayo
yalisemwa juzi na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimatifa, Bernard
Membe, kufuatia swali la mwandishi mmoja wa Malawi aliyetaka kujua msimamo wa
sasa wa Tanzania kuhusu mgogoro huo.
Waziri
Membe alikuwa jijini Blantyre, Malawi, akiongoza ujumbe wa Tanzania
uliosafirisha mwili wa aliyekuwa balozi wa nchi hiyo nchini Tanzania, Flossie
Gomile-Chidyaonga, aliyefariki ghafla jijiji Dar es Salaam ijumaa iliopita.
Mwili huo ulisafirishwa kwa ndege ya serikali ilyotolewa na Rais Jakaya
Kikwete, jambo ambalo limewakuna wananchi wa Malawi wakiipongeza hatua hiyo.
"Kama
wote mnavyojua, Tanzania na Malawi zilimua kupeleka suala hili kwenye jopo
linaloongozwa na Rais wa zamani wa Msumbiji, Joachim Chisano, akisaidiwa
na Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki na Rais wa Mstaafu wa Botswa,
Festus Mogae.
"Tulichukua
uamuzi huu kutokana na uhusiano mzuri wa kindugu ambao nchi zetu, Tanzania na
Malawi, tunao, kwamba badala ya kubishana sisi wenyewe kwa wenyewe tukipe
chombo kingine kutazama mgogoro wenyewe na kutoa uamuzi," alisema.
Alisema
kwa kuwa Malawi inafanya uchaguzi wake mkuu, jopo la marais hawa wa zamani
liliona lisubiri uchaguzi huo kumalizika. Alisema baada uchaguzi, serikali
itakayoingia madarakani, iwe ya sasa inayoongozwa na Rais Joyce Banda ama ya
sura nyingine, basi suala hilo litazungumzwa tena katika awamu ya pili.
"Ni
matumaini yetu kwamba jopo la wazee wetu hawa kwa kushirikiana na wanasheria
waliobobea, watatupeleka sehemu ambayo tutajua namna nzuri ya kulimaliza suala
hili na tuna imani kwamba sisi kama ndugu ambao tumekuwa tukilitumia ziwa hili
karne kwa karne suala hili litapata ufumbuzi mzuri," alisema.
Alisema
kwa sasa mtazamo wa Tanzania umejikita kwenye maana ya "mpaka baina ya
nchi na nchi unaotokana na ziwa (mto ama bahari)."
"Hata
mki-google (mkitumia injini ya google ya kutafutia habari kwenye mtandao)
mtaona kwamba uamuzi wa mpaka wa Tanzania na Malawi katika eneo hili bado
haujawahi kufikiwa. Kwa vile hayajawahi kuwepo mazungumzo ya kujadili mpaka
uweje, kinachotakiwa, kwa mantiki hiyo, ni nchi hizi kuunda tume za mpaka kwa
pamoja, kuangalia na kisha kukubaliana ni wapi mpaka kwenye ziwa hili uwe, kama
ni katikati ama vinginevyo katika namna ambayo inakubaliwa kimataifa,"
alisema.
Mgogoro
wa ziwa Nyasa ambao hata hivyo ulikuzwa sana na vyombo vya habari kuliko hali
halisi, ulikuja baada ya Malawi kudai kwamba ziwa hilo lote liko nchini Malawi
na kwamba mpaka ni ufukweni kwa upande wa Tanzania.
Dai
hili lilileta mtazamo kwamba kwa upande wa Tanzania, mpaka ni pale yanapoanzia
maji ya Ziwa Nyasa na hivyo Mtanzania anapovua samaki ama kuteka maji kwenye
ziwa hilo, anakuwa ameingia nchi nyingine ya Malawi.
No comments:
Post a Comment