MGANGA ABAMBWA AKIPIKA MIKONO YA MWANAFUNZI KAGERAWakati jamii ya Watanzania ikipigwa butwaa na ukatili wa kutisha aliofanyiwa mtoto wa miaka minne kwa kufungiwa ndani ya boksi kwa miaka mitatu mjini Morogoro, ukatili mwingine wa kutisha  dhidi ya watoto umeripotiwa mkoani Kagera.
Katika mkoa huo, mganga wa kienyeji ametiwa mbaroni, akituhumiwa kumuua kwa kumnyonga, kumkata mikono na kumzika katika nyumba yake.
Mganga huyo, Mujingwa John (20) amekiri mbele ya jeshi la polisi kuhusika na mauaji ya mtoto Fausta Geofrey (8), mwanafunzi wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Kitunga kata ya Muhutwe, wilayani Muleba.
Anatuhumiwa kwamba, alimkamata kwa nguvu akienda shule na wenzake, akamuua, kumkata mikono, nyama ya mgongo, masikio na sehemu za siri kwa lengo la kuibanika na kutengeneza 'uchawi' wake, kisha akachimba shimo na kuzika mwili ndani ya nyumba.
Tukio hilo lilithibitishwa na Kamanda wa Polisi mkoa wa Kagera, George Mayunga aliyesema mganga huyo alikamatwa na polisi kwa kushirikiana na wananchi, ambapo alikutwa akibanika viungo alivyovikata kutoka kwa mtoto huyo.
Aidha, akiwa polisi, mganga huyo alipewa fursa ya kueleza kilichotokea mbele ya waandishi wa habari, ambapo alidai  alifikia uamuzi wa kumuua mtoto huyo, kutokana na hali ngumu ya umaskini inayomkabili.
Alisema baada ya kumkamata mtoto huyo, alimkaba shingo na kumvuta hadi katika nyumba aliyokuwa akiishi, akamnyonga hadi kufa na baada ya kufa, alimkata ngozi ya mgongoni, mikono akianzia na mkono wa kushoto aliodai una bahati, sehemu za siri na masikio.
"Nilimkamata mtoto na kumuua, maana niliona nikikamata mtu mzima atanizidi nguvu na kupiga kelele," alidai.
Alidai kuwa, "Nilipomaliza kumuua nilichimba shimo chini ya kitanda changu nikamzika na kutandaza nyasi juu yake ili isigundulike kama eneo hilo kuna shimo".
Mganga huyo aliyejitambulisha kuwa ni Msukuma, alidai viungo hivyo ambavyo hadi polisi wanafika, alikuwa bado akivikausha, angevichanganya na dawa ambayo angewapatia wateja wake ili iwasaidie kufanikisha mambo yao, ikiwamo kupata bahati na utajiri na alitarajia kuuza kwa Sh 500 kwa kila ujazo wa kijiko kimoja cha dawa yake.
Alisema hiyo ni mara yake ya kwanza kufanya tukio la aina hiyo na kwamba alihamia Muleba mkoani Kagera miaka miwili iliyopita akitokea Nyanguge wilaya ya Magu mkoani Mwanza. Alisema alirithi uganga huo kutoka kwa babu yake mzaa mama na kuwa alianza uganga akiwa na umri wa miaka minane na hakuwahi kwenda shule.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Bisole katika Kata hiyo wilayani Muleba, Khamis Hassan, akizungumzia tukio hilo baada ya mauaji hayo, alidai muuaji alimkata mtoto huyo mikono yake miwili kabla ya kumzika.
Hassan alisema kuwa tukio hilo ni la Mei 21 mwaka huu asubuhi katika kijiji hicho, wakati mtoto huyo akiwa na wenzake wakielekea shuleni, ambapo inadaiwa aliitwa na kukamatwa na mganga huyo, aliyetambulika kwa jina la Mujingwa John (20).
Alisema kuwa baada ya taarifa za mtoto huyo kutoonekana kuzagaa, wanakijiji walikusanyana na kuanza msako, ambapo walikamata kundi la watu waliokuwa wakiwahofia kuhusika, hasa vijana.
Alisema baada ya kuwakamata watu hao, waliwaweka sehemu moja na kuwaita wanafunzi waliokuwa na marehemu, ambapo walimtambua mganga huyo kuwa ndiye aliyemwita na kumkamata mtoto huyo.
Mtendaji huyo alidai baada ya mganga huyo kutambuliwa, wananchi na polisi waliofika eneo hilo, walikwenda naye hadi katika nyumba anayoishi na kumtaka awaonyeshe alipo mtoto huyo.
Alidai baada ya kumbana, aliwaonesha sehemu alikomzika, ambapo walichukua jembe na kuanza kufukua mwili wa mtoto huyo, uliokuwa umezikwa ndani ya nyumba aliyoishi mganga huyo.
Alidai baada ya mganga huyo kumuua mtoto huyo, alimkata mikono yake miwili na kisha kuchimba shimo ndani ya nyumba, ambapo baada ya kumzika alifukia shimo akatandaza nyasi juu yake na kisha kuweka kitanda chenye godoro alilokuwa akilala.
Alisema kuwa alipohojiwa ili kujua nani kamtuma kutekeleza unyama huo, mganga huyo alidai ilitokana na yeye kuoteshwa na mizimu yake, iliyomtaka kumuua mtoto ili amkate viungo vyake kwa ajili ya kuchanganya na dawa.
Alisema mikono hiyo alitaka kuibanika kwenye moto ili aichanganye na dawa, ambayo angewapatia watu wanaohitaji kupata utajiri.
Tukio hilo limekuja siku chache wakati Jeshi la Polisi mkoani Morogoro, likiendelea na  uchunguzi wa kilichotokea mpaka mtoto mmoja mkoani hapa (jina limehifadhiwa), akateswa na mama mlezi kwa kuwekwa katika boksi tangu akiwa na miezi tisa, mpaka alipotimiza miaka minne.

No comments: