MGAHAWA UNAOZUNGUKA DAR WAKAMATWA KWA KUKWEPA KODI



Mgahawa maarufu jijini Dar es Salaam unaozunguka juu ya  jengo la Golden Jubilee lenye zaidi ya ghorofa 20, umekamatwa kwa kukwepa kodi baada ya kuacha kutumia Mashine ya Kodi ya Kielektroniki (EFDs) licha ya kuwa nayo.
Kutokana na hali hiyo, wamiliki wa mghahawa huo, wametozwa faini ya Sh milioni tatu kwa kuwa ni kosa la kwanza na iwapo watabainika kuendelea kukwepa kodi, watafikishwa mahakamani na hatimaye kufungiwa biashara.
Maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), jana mchana walifika katika mgahawa huo uliopo katikati ya Jiji wakiwa na risiti za kielektroniki zenye jina la Akemi, wanazotoa badala ya zile za TRA na kuuonyesha uongozi wa hoteli hiyo.
Naibu Kamishna wa Idara ya Kodi za Ndani, Generosa Bateyunga, alisema walipata taarifa kutoka kwa wateja wa mgahawa huo, kupewa risiti zao na siyo za TRA ambazo walikuwa wamepata huduma za Sh 175,000.
“Ndipo tuliamua kuwatuma wafanyakazi wetu ambao walilipa na kupewa risiti ambayo siyo ya TRA, na walipojitambulisha walipewa risiti halali, jambo linaloonyesha kuwa wanayo mashine lakini hawatumii kwa wateja wote na hiyo ni kukwepa kodi makusudi,”alisema. 
Alidai mgahawa huo unatoa risiti za kielektroniki zenye jina la mgahawa, lakini siyo za TRA, kwani risiti halali ni zenye nembo ya Mamlaka, jina la Mmiliki, Anuani na mengineyo. Alidai kati ya wateja 10, wanaowapa risiti za TRA ni mmoja.
Alisema mgahawa huo ni kati ya michache yenye viwango vya juu kutokana na kuzunguka, na mlipakodi mkubwa aliyesajiliwa katika orodha ya wafanyabiashara wanaolipa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) hivyo ni lazima itoa risiti za TRA.
Akizungumzia suala hilo, Mkurugenzi Mkuu wa Alcove group ambao ni wamiliki wa mgahawa huo, Sanjay Kanabar, alisema alisaini barua ya kupokea taarifa ya kulipa faini, lakini siyo kweli kwamba hawatoi risiti za TRA, bali inatokana na kusumbua kwa mtandao.
Alisema risiti zao wanazotoa ni kwa ajili ya kumpa bili mteja, lakini mtandao ukikataa, wanawapa kama risiti jambo ambalo wameishatoa taarifa mara kadhaa kwa kampuni iliyowauzia mashine hiyo.

No comments: