MFANYABIASHARA KIZIMBANI KWA KUISABABISHIA HASARA TANESCOMfanyabiashara Ibrahim Mshana, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na mashitaka ya kusababishia Shirika la Umeme (TANESCO) hasara ya Sh milioni 1.4.
Mshana alifikishwa mahakamani hapo na kusomewa mashitaka mawili na Mwendesha Mashitaka Inspekta Jacksoni Chidunda, mbele ya Hakimu Mkazi, Frank Moshi.
Chidunda alidai kuwa Oktoba 15 mwaka huu Ukonga, Mshana aliingilia huduma zinazotolewa na Tanesco kwa kuingiza waya kwenye mita namba 24210835377 katika nyumba ya Azzas Said, mali hiyo ni ya Tanesco ambayo hutumika kwa ajili ya kutoa huduma.
Aliendelea kudai kuwa, siku hiyo hiyo, Mshana alisababisha hasara ya fedha kwa Tanesco baada ya kuingiza waya kwenye mita hiyo.
Mshitakiwa alikana mashitaka na kurudishwa rumande baada ya kukosa wadhamini. Upande wa  mashitaka ulidai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kesi itatajwa tena Mei 29 mwaka huu.

No comments: