Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe ameshauri Watanzania kutokwenda sasa
Libya, kutokana na mgogoro unaoikumba nchi hiyo.
Alisema katika mgogoro wa
Libya, hali ya usalama bado ni tete, jambo lililofanya ofisi za balozi
mbalimbali mjini Tripoli na Beghazi kufungwa.
Membe alisema hayo
jana wakati akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo
mwaka wa fedha ujao ya Sh bilioni 191,919,748,000.00.
Aidha, alitoa msimamo wa
Serikali juu ya mgogoro wa Ukraine na kusema Tanzania haitafungamana na upande
wowote.
Alisema hatua hiyo,
inalenga kuepuka kuingia kwenye mgogoro huo unaotishia amani na usalama
wa dunia kwa kuirudisha tena kwenye vita baridi.
Membe alisema
kuhusu mgogoro wa Ukraine unaotishia kuigawa dunia katika pande mbili kwa
zinazounga mkono kujitenga kwa jimbo la Crimea zikiongozwa na Urusi na
zinazopinga zikiongozwa na mataifa ya Ulaya na Marekani.
Alisisitiza, “msimamo wa
Tanzania ni kutofungamana na upande wowote na inaendelea kuiomba Jumuiya ya
Kimataifa kushughulikia mgogoro huo kwa kutumia hekima na busara ambayo
itaiepusha dunia kuingia kwenye vita.”
Akizungumzia uraia wa
nchi mbili, Membe alisema, “suala hili tayari limewekwa kwenye rasimu ya
Katiba mpya na tutajadili kwa nguvu za hoja na kwamba umefikia wakati wa nchi
yetu kuwa na sheria ya kuruhusu uraia pacha kwa maendeleo na maslahi ya
taifa na matumaini yangu ni kuwa Bunge litaunga mkono pendekezo
hilo.”
Kuhusu mgogoro wa Malawi,
Waziri Membe alisema kwa sasa Wizara inaandaa majibu kwenye jopo la usuluhishi,
kueleza hasara tutakazopata endapo itaamriwa kuwa mpaka upite kwenye ufukwe wa
Ziwa Nyasa.
Hatua hiyo imetokana na
jopo hilo linaloongozwa na Rais mstaafu wa Afrika Kusini ,Thabo Mbeki
kushauri hoja za kisheria kuwekwa pembeni na kujadili hoja zinazogusa
maisha ya kila siku ya kijamii.
No comments:
Post a Comment