MBWAMWITU, WATOTO WA MBWA NA PANYA ROAD KUTOKOMEZWAJeshi la Polisi nchini limewaagiza Makamanda wa Polisi wa Mikoa, kuhakikisha wanavidhibiti na kuvitokomeza vikundi vyote vinavyojihusisha na vitendo vya uhalifu, ikiwemo uporaji, unyang'anyi na kujeruhi watu katika maeneo mbalimbali.
Agizo hilo limetolewa na Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi Nchini (DIGP), Abdulrahman Kaniki.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso, hatua hiyo imetokana na kushamiri kwa matukio ya uhalifu na yanayojenga hofu miongoni mwa jamii, ikiwa ni pamoja na vikundi vinavyozidi kuibuka na kutishia amani katika Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.
Vikundi hivyo ni pamoja na vile vilivyojipachika majina ya mbwa mwitu, watoto wa mbwa au panya road, ambavyo vimekuwa vikifanya uporaji, unyang'anyi wa kutumia nguvu na kuwajeruhi watu katika maeneo mbalimbali.
Makamanda hao wametakiwa kuhakikisha wanavitafuta vikundi hivyo popote vilipo na kuwakamata kisha kuwafisha katika vyombo vya sheria.
"Naibu IGP amekemea vikali vikundi hivyo na kuvitaka kuacha tabia hiyo mara moja, kwani vitendo hivyo ni vya kihalifu na vinatakiwa kukemewa na kila mtu katika jamii," ilieleza taarifa hiyo ya Senso.
Aidha, iliwataka wananchi kuondoa hofu na badala yake watoe ushirikiano kwa kutoa taarifa za vikundi hivyo katika vituo vya Polisi ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa.

No comments: