MBUNGE WA CHADEMA AWAACHA VINYWA WAZI WENZAKEMbunge wa Viti Maalumu, Leticia Nyerere (Chadema) ameeleza kufurahishwa na Serikali kwa kufanyia kazi maombi yote ambaye amekuwa akiyawasilisha bungeni, miongoni mwake ikiwa ni pamoja na wananchi wa Kwimba kupatiwa huduma za kijamii. 
Leticia ambaye alikuwa akichangia makadirio ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2014/15, alisema juzi kwamba aliomba maji, walimu, umeme na mawaziri husika wamempatia . 
“Naipongeza Serikali ya CCM kwa kutekeleza yale yote ambayo nimekuwa nikiyapigania bungeni.,” alisema Leticia ambaye alisisitiza umuhimu wa wananchi kuchangia miradi ya maendeleo. 
Akizungumzia maombi yake kuhusu walimu, alisema halmashauri ya wilaya ya Kwimba imepatiwa walimu 300. 
Hata hivyo aliendelea kuwasilisha maombi ya vitabu kwa ajili ya shule wilayani humo. Alisema idadi  hiyo ya walimu  ni sawa na kuvaa suruali bila kufunga vifungo.  
Leticia ambaye uchangiaji ulionekana kuduwaza upande wa upinzani wakati upande wa CCM wakishangilia, alimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,  Evarist Ndikilo pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Kwimba,  Seleman Mzee kwa uchapakazi wao. 
Baada ya kuchangia, alishangiliwa na wabunge wa CCM na Spika Anne Makinda alisema, “Kushukuru ni kuomba…na hiyo ndiyo siasa.” 
Katika hatua nyingine     Mbunge wa Viti Maalumu, Magdalena Sakaya (CUF) alikosoa  hatua ya serikali kuonesha silaha zake katika maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano.  Alishutumu kitendo hicho akisema si haki nchi kuonesha silaha zake hadharani. 
Hata hivyo Mbunge wa Manyoni Mashariki, John Chiligati (CCM), alimpa taarifa akisema kilichooneshwa ni kitu kidogo.  Chiligati alimwambia kuonesha silaha ni jambo la kawaida duniani. 

No comments: