MBOWE KUUNDA UPYA 'BARAZA LA MAWAZIRI' BUNGENI

Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe amesema anatarajia kuvunja na kuunda upya Baraza la Mawaziri Vivuli, litakaloshirikisha viongozi wengine wa vyama vya upinzani, wanaounda kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).
Aidha, alisisitiza kasi ya Ukawa katika kuizunguka nchi na kufanya mikutano mbalimbali, kamwe haijapungua.
Alisema hayo juzi katika viwanja vya Gombani ya Kale mjini Chake Chake kisiwani  Pemba, ambako viongozi wa Ukawa walifanya mkutano wa hadhara, kuelezea mambo mbalimbali kuhusu mchakato wa Katiba mpya.
Mbowe alisema umoja huo unatarajia kuwaungunisha watanzania ili wapate Katiba mpya, inayotokana na maoni na kuzingatia maslahi yao.
Alifahamisha kuwa umoja huo una dhamira ya kweli na kwamba kuanzia sasa hawatakuwa tayari kugawanywa kwa misingi udini, ukabila au maeneo.
Mbowe ambaye ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, alisema kwa kipindi kirefu vyama vya upinzani vimekuwa vikibaguliwa kwa misingi hiyo. Aliahidi kuwa vitendo hivyo, sasa vimefikia mwisho.
“Sisi Chadema tumezushiwa propaganda kuwa ni chama cha Kikristo, na wenzetu wa CUF wakaambiwa kuwa ni chama cha Kiislamu. Sasa tumegundua kuwa lengo lao ni kutugawa na sasa hatugawiki tena,” alisisitiza Mbowe.
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba alirejea kauli zake kuhusu matumizi mabaya ya fedha za umma ndani ya serikali. Alisema kwamba kama vitendo hivyo vitaachwa viendelee, nchi itashindwa kupiga hatua za maendeleo kwa haraka.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia ambaye pia ni Mbunge aliyeteuliwa na Rais Jakaya Kikwete, alisema kitendo cha baadhi wa viongozi wa serikali, kudai kwamba iwapo muundo wa serikali tatu utakubaliwa, Zanzibar itakuwa dola ya Kiislamu ni chokochoko, ambazo hazina ukweli.
Alisema Waislamu na Wakristo wa Zanzibar, wana uhusiano wa muda mrefu na wa kihistoria, ambao hauwezi kutenganishwa.
Alielezea historia ya kanisa la Minara Miwili la Zanzibar, ambalo ni miongoni mwa makanisa yenye historia ndefu katika Afrika Mashariki.

No comments: