MBARONI KWA MADAI YA KUMUUA DEREVA BODABODA

Polisi mkoani Katavi inawashikilia watu watatu wakituhumiwa  kumuua kikatili kwa kumchinja  dereva  wa pikipiki  ‘bodaboda’ Frank Joseph (25)  mkazi  wa Mtaa wa Nsemulwa  mjini Mpanda kisha  kumpora  pikipiki  yake.
Kamanda  wa Polisi  wa Mkoa  wa Katavi, Dhahri  Kidavashari  akizungumza kwa njia ya  simu  jana  kutoka mjini  Mpanda  aliwataja  watuhumiwa kuwa ni Charles  Kidaha (29), Madia Mtema (40) na Buyenza  Jendesha (40) wote wakazi wa Kijiji  cha Mwese  wilayani Mpanda.
Kidavashari  alidai  tukio hilo  lilitokea   Aprili  26, mwaka huu, saa  saa 11 jioni kijijini Mpembe  katika Tarafa ya Mwese  wilayani Mpanda.
Akisimulia Kamanda Kidavashari  alidai kuwa  siku  ya tukio  marehemu akiwa na pikipiki   aina ya  SunLG  yenye nambari za  usajili  T 704 CDQ, alikodiwa na mtu asiyefahamika kwenda mahala kusikojulikana na kesho yake mwili wake ulionekana ukiwa umetelekezwa  porini  karibu na kijiji cha  Mpembe.
Alisema uchunguzi wa Polisi ulibaini kuwa kifo cha dereva huyo kilitokana na kuchinjwa na watu wasiofahamika ambao baada ya kitendo hicho walitoweka  na pikipiki hiyo.

No comments: