MAWAZIRI MIRADI YA MATOKEO MAKUBWA KUJIELEZA KWA JKIkiwa ni takribani mwaka mmoja sasa tangu Serikali ilipoamua kuanza kutekeleza Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), hatimaye mawaziri wanaotekeleza Mpango huo watawekwa `kikaangoni’ Julai mwaka huu.
Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam  mwishoni mwa wiki na Mtendaji Mkuu wa Kitengo cha Rais Kinachosimamia Utekelezaji wa Mpango huo (PDB),  Omari Issa alipokutana na watendaji wakuu kutoka taasisi za umma na binafsi.
PDB iliundwa rasmi Julai mosi mwaka jana kwa lengo la kusimamia utekelezaji wa miradi mikubwa sita ya kipaumbele katika sekta za elimu, kilimo, usafirishaji, nishati, maji na ukusanyaji wa mapato.
“Kazi hii tumeshaitekeleza kwa takribani miezo 10, tunajiandaa kufanya tathmini ya kina ya utekelezaji ambapo Julai mwaka huu, mawaziri wote waliosaini mikataba mbele ya Rais Jakaya Kikwete watahojiwa, watapimwa na matokeo kuwekwa hadharani,” alisema Issa.
Alisema, BRN ni utamaduni unaojaribu kujenga uwajibikaji, uwekaji wa vipaumbele na kisha kutekeleza mipango husika kwa wakati bila urasimu uliozoeleka katika sekta nyingi.
Akizungumzia mchakato huo wa kuwapima mawaziri hao utakavyokuwa, alisema, shughuli hiyo itaanza kwa mawaziri hao mmoja mmoja kukutanishwa na Rais ambapo atawahoji kwa kina kuhusu kazi walizopewa na watajieleza.
Mchakato huo utafuatiwa na timu huru ya tathmini itakayohusisha wataalamu mbalimbali kutoka nje ya nchi ambao nao wataangalia na kuhakiki utendaji wa mawaziri husika kwa mujibu wa mikakati waliyopewa kuitekeleza chini ya BRN.
“Zoezi hili litakuwa la wazi kwa kadiri itakavyowezekana, wananchi wataambiwa nini BRN imeweza kutekeleza na kipi hakikutekelezwa na sababu zake, ” alisema Issa.
Hata hivyo , alisema mara baada ya kuhojiwa kwa mawaziri hao mbele ya Rais, (Rais) ndiye mwenye mamlaka ya kuwachukulia hatua ikiwa ataona kuna haja ya kufanya hivyo kwa kuwa ndiye aliyewateua.
Akizungumzia mafanikio ya BRN mpaka sasa, Issa alitaja kuanza kujengeka kwa utamaduni wa watu kuwajibika, kuweka mipango na  kuitekeleza kwa wakati hata kama miradi hiyo haipo moja kwa moja chini ya BRN.
Alitaja mfano wa sekta ya usambazaji wa maji kuwa ndani ya miezi 10, tu ya kuanza kwa BRN, zaidi ya Watanzania milioni 2.5 wamefikishiwa huduma hiyo hadi vijijini, wakati kabla ya BRN, kati ya watu laki tatu hadi tano ndio waliokuwa wakifikishiwa huduma hiyo muhimu.
Watendaji wakuu wengi wa taasisi na mashirika waliohudhuria walieleza kuridhishwa na  BRN na kuahidi kushirikiana nayo katika kuleta maendeleo ya Taifa.
Tanzania imeanza kutekeleza mfumo wa BRN Julai mwaka 2013, wenye lengo la kuleta maendeleo na kuifanya nchi kuwa yenye uchumi wa kati kutoka wa chini na kuwa mfumo huu, uliochukuliwa nchini Malaysia.
Malaysia wao mfumo huo umeonesha mafanikio makubwa na sasa ni moja ya nchi iliyoendelea kiviwanda na iko kwenye rekodi nzuri za nchi zenye uchumi wa juu barani Asia, na inategemewa ifikapo mwaka 2020 itakuwa ni moja ya nchi zilizoendelea.
Malaysia wakati ikipata uhuru wake, ilikuwa na uchumi sawa na wa Tanzania, lakini sasa kupitia BRN, mapinduzi ya maendeleo yameonekana na uchumi wao unaendelea kukua kwa kasi.
Mfumo huo kuanza kutekelezwa hapa nchini, unaweza  kufanikiwa kwa kuwa nchi ya Malaysia nayo  ilikuwa na rasilimali zinazofanana na za Tanzania kama vile sekta ya  madini na kilimo, ambazo ndizo gurudumu la maendeleo. Nchi nyingine za Afrika zilizofuata mfumo huo ni Rwanda na Nigeria.

No comments: