MATOKEO YA UTAFITI WA CHANJO YA UKIMWI KUTOLEWA LEO



Matokeo ya utafiti wa chanjo ya ugonjwa wa Ukimwi na magonjwa yasiyoambukizwa nchini, yatatolewa katika kongamano la kisayansi linaloanza leo jijini Dar es Salaam.
Kongamano hilo la siku mbili lenye kauli mbiu ya ‘Utafiti wa Afya, Mafunzo na Ubunifu kwa Maendeleo Endelevu’, limeandaliwa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas).
Kaimu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Eligius Lyamuya, alisema juzi Dar es Salaam kwamba utafiti huo utatolewa mbele ya wanasayansi washiriki 350 toka nchi tisa duniani, ambao watatumia kongamano hilo kubadilishana ujuzi na uzoefu katika ufanyaji utafiti.
Mada zaidi 138, zinatarajiwa kuwasilishwa katika kongamano hilo, ambapo kati ya hizo mada 122 zitawasilishwa kwa njia ya mdomo, ikiwemo ya utafiti wa chanjo ya Ukimwi pamoja na magonjwa yasiyoambukiza.
Mwaka jana Kiongozi wa Jopo la Wataalamu wa Muhas wanaofanya utafiti huo, Profesa Muhammad Bakari, alitoa ufafanuzi kuhusu majaribio ya chanjo hiyo, akisema bado walikuwa wakiendelea kuifanyia utafiti zaidi.
Profesa Bakari alikaririwa akisema majaribio ya chanjo hiyo yaliyofanyika nchini mwaka 2007 mpaka 2010 na 2008 mpaka 2012, yalionyesha mafanikio mazuri, ingawa hayakufikia hatua ya kupatikana kwa chanjo kamili.
Kwa mujibu wa Profesa Bakari majaribio hayo yalithibitisha kuwa chanjo ya DNA – MVA, ilikuwa salama na yenye uwezo wa kuufanya mwili utengeneze kinga dhidi ya virusi vya Ukimwi (VVU).
Pamoja na matokeo hayo ya kutia moyo, baada ya kuanza kufanya utafiti, jopo la madaktari bado liliendelea na utafiti zaidi ulioanza 2008 hadi 2012 ili kupata chanjo.
“Hatukuishia hapo, utafiti wa pili (TAMOVAC-01), ulifanyika kati ya  2008 na 2012. Utafiti huu ulijumuisha pia nchi jirani ya Msumbiji,” alisema.
Alisema utafiti wa awali ambao uliojulikana kama HIVIS-03, ulihusisha askari 60 ambao walifuatiliwa kwa karibu wakati wote wa utafiti, ili kuhakiki usalama wa chanjo na uwezo wa chanjo kutengeneza vichocheo vya kinga dhidi ya VVU.
Profesa Lyamuya alisema mada nyingine ni pamoja na maendeleo katika kushughulikia Malengo ya Maendeleo ya Milenia katika suala la afya, utafiti wa mifumo ya afya na nyinginezo.
“Kongamano hilo litatumika kuhamasisha matokeo ya utafiti, ili yatumike na watekelezaji, wadau wa afya, watoa huduma wa afya na wengine wanaofanya kazi katika maeneo husika ya kitaaluma,” alisema Profesa Lyamuya.
Wataalamu hao mbali na kutumia kongamano hilo kubadilishana mawazo na ujuzi kuhusu utafiti mbalimbali, pia wataweka mikakati mbalimbali kwa wadau wa ndani na nje ya nchi, kuhusu kutumia utafiti mbalimbali wa afya kuboresha utoaji huduma za afya, ikiwemo kuwa na vifaa madhubuti.
Kongamano hilo ni la pili kufanyika nchini na kuendeshwa na chuo hicho, ambapo mwaka jana makala za kisayansi 144, ziliwasilishwa na kusaidia utoaji huduma za afya pamoja na kutunga sera kukabiliana na changamoto za kiafya.

No comments: