MASHINE ZA XRAY ZA OCEAN ROAD KUTENGENEZWA WIKI HIIMafundi na vifaa kutoka nchini Canada kwa ajili ya kutengeneza ya mashine  mbili za mionzi zilizoharibika katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, watawasili nchini wakati wowote na matengenezo hayo yatagharimu Sh milioni 740.
Imeelezwa matengenezo hayo, yatachukua siku nne na tayari serikali imelipa Sh 365,046,000 ikiwa ni nusu ya gharama zinazotakiwa.
Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Kebwe Stephen Kebwe aliliambia bungeni jana wakati akitoa kauli ya serikali kuhusu hali ya mashine za mionzi za taasisi hiyo ya Ocean Road.
Alisema mashine zinazotoa tiba ya mionzi katika taasisi hiyo ni mbili na hutibu asilimia 95 ya wagonjwa wa saratani na wanaohitaji mionzi  na nyingine ndogo inayotumika kwa wagonjwa wachache, hasa wenye saratani ya ngozi.
“Kwa kawaida mashine hizi zinatakiwa kufanyiwa matengenezo kila baada ya miezi mitatu, aidha mafundi wa kutengeneza mashine hizo wanatoka nje ya nchi hivyo kuharibika kwa mashine hizo kunasababisha wagonjwa kukosa huduma kwa muda” alisema
Kebwe alitaja mashine zinazohitaji matengenezo ni Equinox no 2002, ambayo chanzo chake cha mionzi bado ni kizima, lakini imeharibika na Equinox no 2004  inayohitaji chanzo kipya cha mionzi.
Alisema mtengenezaji pekee wa mashine hizo ni kampuni ya Theratronics kutoka Canada na ilipewa zabuni kutengeneza mashine hizo.
“Kampuni hiyo itatakiwa kuharibu vyanzo vyote vya mionzi vitakavyotokana na utengenezaji wa mashine hizo za mionzi na ubadilishaji wa vyanzo vya mionzi, ufungaji wa vipuri vipya na kubeba masalia yote ya vipuri kutoka mashine zote mbili na kurudisha nchini Canada ili kudhibiti isilete madhara kwa watanzania,” alisema.
Naibu waziri huyo alisema mwaka 2013/2014 taasisi hiyo ilihudumia wagonjwa 4,712 wa saratani, ikiwa ni ongezeko la wagonjwa 976, ikilinganishwa na kipindi cha mwezi Julai hadi Machi mwaka 2012/2013.
Alisema wagonjwa 3,295 walitibiwa kama wagonjwa wa nje na 1,417 walilazwa  huku wanawake 4,985 walifanyiwa uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi na matiti. Kati ya hao wanawake 197 waligundulika na dalili za awali za saratani ya kizazi na 61 walikuwa na dalili za kuwa na saratani ya matiti.
“Nia ya serikali ni kuona mashine hizo zinaanza kufanya kazi mapema iwezekanavyo ili wananchi waendelee kupata huduma hizo za mionzi,vile vile serikali itaajiri Biomedical Engineers katika hospitali zetu za rufaa ikiwemo ORCA ili waweze kushirikiana na kupata elimu kutoka kwa wataalamu hawa kutoka Canada watakaofika kutengeneza ili baadaye kujenga uwezo wa kufanya matengenezo kinga wenyewe,” alisema Kebwe.

No comments: