MAPYA YAIBUKA KUHUSU KIFO CHA MWIGIZAJI ADAM KUAMBIANA

Wakati mwili wa mwigizaji na mwongozaji mahiri wa filamu hapa nchini, Marehemu Adam Philip Kuambiana ukizikwa kwenye makaburi ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam jana, mapya yameibuka kuhusu kifo chake kulichotokea Jumamosi iliyopita.
Taarifa hizo zimeleta tafsiri kwamba huenda Kuambiana alifahamu kwamba yuko mbioni kuaga dunia katika siku chache zinazofuatia kutokana na ishara nyingi alizokuwa akionesha kwa watu wake wa karibu aliokuwa akifanya nao filamu.
Kuambiana alifariki kutokana na kile kilichoelezwa maradhi ya sukari na vidonda vya tumbo, ambapo siku hiyo ya Jumamosi alianguka ghafla na kukimbizwa Hospitali ya Mama Ngoma iliyoko maeneo ya Mwenge, Dar es Salaam ambapo ilithibitika alifariki dunia kabla ya kufikishwa hapo.
Mmoja wa watu aliokuwa akifanya nao filamu siku chache kabla ya kufikwa na umauti, William Mtitu, alielezea ishara ambazo Kuambiana alikuwa akionesha wakati wakiandaa moja ya filamu zake ambazo sasa amebaini kwamba alikuwa akitabiri kifo chake.
Mtitu alisema kwamba, wakati wakiendelea ku-shoot 'scene' mojawapo, Kuambiana alishindwa kabisa kuendelea na zoezi hilo kwa siku hiyo na hivyo yeye (Mtitu) kumruhusu aende hospitali kwa ajili ya kuchekiwa vipimo kutokana na kulalamika mno maumivu ya tumbo.
"Wakati tukiwa tunamalizia kazi hiyo, Kuambiana alionekana kutulia dakika kadhaa bila kuongea chochote na hatimaye akasema neno moja tu, Niombeeni!" alisema Mtitu kwa uchungu.
Mtitu alisendelea, "Mie kwa uzoefu wangu nikafikiri kwamba yeye kama Mwongozaji alitumia kauli hiyo kujaribu kuwapa moyo wasanii wengine walioonekana kuchoka mno waweze kujitahidi kumalizia kazi, lakini kumbe haikuwa hivyo alikuwa akituaga. Inauma sana."
Ishara nyingine ni ile aliyoonekana katika kipande kimojawapo cha 'Behind the Scene' ya moja ya filamu zake za hivi karibuni kilichorushwa kwenye kipindi cha TAKE ONE cha CloudsTV, ambapo Kuambiana alishindwa kufanya kile alichotakiwa kufanya na badala yake akafunika uso wake kwa mikono na kumtoka maneno "It's not me!" akimaanisha "si yeye" kutokana na akili yake kuwa mbaali kabisa kwa mawazo.
Akihojiwa na CloudsTV msibani, mwigizaji wa kike aliyefanya filamu na Kuambiana wiki moja iliyopita, Mariam alisema kwamba marehemu ni kama alikuwa akifahamu mauti yalikuwa karibu mno kumfika.
Mariam alisema wakati fulani wakiwa kwenye vyumba vya kubadilishia nguo, Kuambiana alimwambia: "You're my best Actress! Nataka kukupa zawadi." Na baada ya kusema hivyo, Kuambiana akampa shati lake.
"Mimi nikamwambia, sihitaji zawadi yake hiyo ya shati, lakini yeye (Kuambiana) akasisitiza kwa kusema: "Chukua Mariam, huu utakuwa ukumbusho wako siku moja!", alisema Mariam huku akibubujikwa na machozi.
Aliendelea Mariam, "Kumbe kweli sasa lile shati limekuwa ukumbusho wangu kwa Kuambiana. Siamini kwakweli, inaniuma sana"
Wakati wa kuaga mwili wa marehemu katika viwanja vya Leaders Club, msanii nguli Jacob Steven 'JB' alishindwa kujizuia na kushindwa kumalizia kusoma wasifu wa marehemu kwa kuangua kilio kilicholazimu waliokuwa karibu naye kumpa msaada wa kumwinua.
Alipoinuliwa, JB alimalizia kwa kusema: "Kuambiana ulikuwa mkono wangu wa kushoto, nimebaki peke yangu", huku akibubujikwa machozi.
Naye Mwenyekiti wa Bongo Movie Unity, Steve Mengele 'Steve Nyerere' alishindwa kujielewa wakati akisoma risala fupi kuhusu marehemu Kuambiana na kujikuta akisema maneno bila mpangilio yanye kumsifu marehemu kwa kazi yake.
Marehemu Adam Kuambiana ambaye alizaliwa Juni 6, 1976, ndiye alikuwa nguzo kubwa ya kampuni ya filamu ya Jerusalem inayomilikiwa na JB ambapo kwa mujibu wa mmiliki, Kuambiana alishiriki kuongoza filamu zaidi ya asilimia 75 ya kazi zote za JB.
Filamu yake ya kwanza kuigiza na kuongoza akiwa na kampuni ya Jerusalem ilikuwa Regina, ambapo marehemu alitamba vilivyo na kuifanya iweze kutikisa anga la filamu nchini na Afrika Mashariki.
Wito wa blogu hii: Wasanii wa filamu muendelee kushikamana na pia mfanye juhudi ya kwenda kucheki afya zenu mara kwa mara.

No comments: