MAPENDEKEZO KUPUNGUZA MISAMAHA YA KODI MWEZI UJAO



Serikali imepanga kuleta mapendekezo makubwa ya kupunguza misamaha ya kodi katika bajeti yake inayotarajiwa kusomwa mwezi ujao.
Taarifa hiyo ilitolewa mjini Dodoma jana na Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge Ngara, Deogratias Ntukamazina (CCM).
Katika swali lake Ntukamazina alitaka kujua mkakati wa Serikali wa kuongeza mapato yatakayowawezesha kuwaongezea watumishi wake mishahara na pensheni.
Mwigulu aliwataka wabunge kuyaunga mkono mapendekezo hayo ambayo yatasaidia kuongeza mapato ya Serikali.
“Serikali pia ina mpango wa kuleta bungeni sheria itakayowezesha kuwepo kwa utaratibu bora wa ukusanyaji kodi na kudhibiti ukwepaji wa kodi,” alisema Mwigulu.
Awali akijibu swali la msingi la Mbunge huyo Mwigulu alisema  moja ya
vigezo vya kuboresha maslahi ya wafanyakazi wa umma na wastaafu ni ongezeko la mapato ya Serikali.
“Uzoefu unaonyesha kwamba kasi ya ongezeko la mahitaji ya jamii na maendeleo  ni kubwa kuliko ongezeko la mapato.
“Kwa mantiki hii imekuwa ni changamoto ya kuongeza pesheni kwa wastaafu sambamba na ukuaji wa uchumi.
“Hata hivyo Serikali itaangalia uwezekano wa kuboresha viwango vya pensheni kwa nia ya kuhuisha ili wastaafu waweze kupata unafuu wa maisha,” alisema Mwigulu.
Katika swali lake Ntukamazina aliitaka Serikali iongeze kiwango cha pensheni kwa wastaafu.

No comments: