MANUFAA YA MWEKEZAJI KIWANDA CHA SARUJI MTWARA HAYA HAPA



Rais Jakaya Kikwete amejionea manufaa wanayopata wananchi waliozunguka kiwanda kikubwa cha saruji duniani, ikiwemo kujengewa nyumba, kupata huduma za uhakika za umeme, maji na vijana wao kupelekwa shule.
Kiwanda hicho, Dangote Cement Obajana Plant, kinamilikiwa na tajiri mkubwa zaidi wa Afrika, Aliko Dangote, ambaye pia anajenga kiwanda cha saruji kikubwa kuliko vyote Afrika Mashariki na Kati katika Kijiji cha Hiari Kata ya Namayanga, mkoani Mtwara.
Rais Kikwete katika siku yake ya mwisho ya ziara yake ya siku tatu nchini Nigeria, Ijumaa iliyopita, aliamua kutembelea kiwanda hicho katika eneo la Obajana, Jimbo la Kogi, kilometa 400 Kaskazini Mashariki mwa mji maarufu wa kibiashara wa  Lagos.
Alipokewa kwenye uwanja wa ndege wa kiwanda hicho na   Dangote mwenyewe, ambaye pamoja na mambo mengine alimuelezea manufaa wanayopata wananchi wanaokizunguka.
Alimuelezea Rais Kikwete kwamba kampuni yake inashiriki kwa karibu shughuli za jamii zinazozunguka kiwanda hicho.
Miongoni mwa shughuli hizo kwa mujibu wa Dangote, ni pamoja na kutoa huduma za elimu kwa watoto na vijana wa wananchi wanaozunguka eneo hilo.
Katika kuboresha huduma hizo za elimu, Kampuni ya Saruji ya Dangote inajenga taasisi kubwa ya elimu ya Dangote Academy, ambayo itatoa elimu na mafunzo ya ufundi kwa ajili ya kuandaa wafanyakazi wa kiwanda hicho na watoto wa jamii inayozunguka kiwanda hicho.
Pia wananchi hao na familia zao, wananufaika na huduma za maji na umeme, na tangu kiwanda kianzishwe mabenki 13  yalianzisha matawi yake katika eneo la kiwanda.
“Mheshimiwa Rais, mbali na nyumba za wafanyakazi, tunawajengea hata nyumba za kuishi wananchi wanaozunguka eneo hili ambao wanatuunga mkono sana,” alisema Dangote
Rais Kikwete ambaye alikuwa nchini Nigeria kuhudhuria Kongamano ya Uchumi Duniani-Afrika (WEFA) mwaka huu, mbali na kujionea na kupata taarifa za manufaa kwa wananchi waliozunguka uwekezaji huo, pia alipata taarifa na kujionea uwekezaji wa kiwanda hicho kikubwa cha saruji duniani.
Mbali na uwanja wa ndege wa kiwanda ambako Rais alipokewa na Dangote mwenyewe, pia  alitembelea machimbo ya kiwanda hicho ambayo yako kilometa tisa kutoka kiwandani, ambako malighafi ya kiwanda hicho husafirishwa kwa madaraja na mikada maalumu hadi kiwandani.
Dangote alimwambia Rais Kikwete kuwa kwa sasa kiwanda hicho cha Obajana, kinazalisha tani za kimetriki milioni 10.25 kwa mwaka na kukifanya kuwa kiwanda kikubwa zaidi cha saruji duniani kilichoko katika eneo moja.
Pamoja na kufikia hadhi hiyo ya dunia, Dangote alimweleza Rais Kikwete kwamba bado upanuzi wa kiwanda hicho unaendelea na ukimalizika, uwezo wake wa uzalishaji utaongezeka na kufikia tani za kimetriki milioni 13 kwa mwaka ifikapo mwakani 2015.
Upanuzi huo kwa mujibu wa Dangote ukimalizika, utakuwa umegharimu dola za Marekani bilioni 2.5, na biashara yake itaongezeka kuzidi ya sasa ambayo ina thamani ya dola za Marekani bilioni mbili kwa mwaka.
Kiwanda hicho kilianza kujengwa 2003 na kukamilishwa 2006 ambapo kilizinduliwa na Rais Olusegun Obasanjo Mei 12,  2007, wiki mbili kabla ya kustaafu urais wa Nigeria, kinaajiri watu 800 kwa wakati mmoja na kuwa miongoni mwa waajiri wakubwa zaidi Nigeria.
“Mheshimiwa Rais, ili kuelewa vizuri mchango wa kiuchumi na kijamii za kiwanda hiki na viwanda vyetu vingine katika maeneo mengine ya Nigeria, unahitaji kukumbuka kuwa kabla ya kuanza kujenga kiwanda hiki, Nigeria nzima ilikuwa na uwezo za kuwazalisha tani za kimetriki za saruji milioni 1.5 tu.
“Sasa tunataka kufikia hatua ya kuhakikisha kuwa eneo la Afrika Magharibi na hata bara letu la Afrika, linaacha kabisa kuagiza saruji nje ya bara letu. Na tutafikia huko,” alisema.
Dangote alisema ili kuwa na uhakika wa umeme, uongozi wa kiwanda hicho uliamua kuzalisha umeme wake kwa ajili ya kiwanda hicho kwa kujenga, miongoni mwa hatua nyingine, bomba ya kilomita 92 la kusafirisha gesi kutoka Ajaokuta hadi kwenye kiwanda hicho.
Alipoulizwa na Rais Kikwete kama wanategemea kwa namna yoyote umeme wa Gridi ya Taifa, Dangote alijibu kwa furaha, “hatujaunganishwa kwenye Gridi ya Taifa na tunadhani hili ni jambo zuri kwa sababu hatua tulizochukua zinatuhakikishia umeme wakati wote na kwa kiwango ambacho tunakihitaji.
“Tunatumia gesi ama dizeli yetu wenyewe. Na wala siyo umeme tu, hata miundombinu ya eneo hili  ikiwemo daraja hili kubwa linalonganisha eneo la machimbo na kiwanda, tumejenga sisi Mheshimiwa Rais,” alisema Dangote.
Mbali na kujenga miundombinu ya umeme wake, Dangote alisema kiwanda hicho pia kimejenga bwawa lake lenyewe kwa ajili ya huduma ya maji kusaidia uzalishaji wa saruji bila kutegemea huduma ya maji ya Serikali.
Bwawa hilo, ndilo linalotoa huduma ya maji kwa jamii inayozunguka kiwanda hicho.
Ili kuhakikisha kuwa upanuzi wa kiwanda hicho unakwenda kwa kasi kubwa zaidi, Dangote ameagiza malori 6,000 kutoka China kusaidia ujenzi na pia ameagiza maelfu ya vibarua kutoka nchi hiyo hiyo ya China, kwenda kushiriki katika ujenzi huo na kuumaliza kwa haraka.
Dangote alimwambia Rais Kikwete kuwa kampuni yake inafanya jitihada kubwa kuhakikisha anakifungua kiwanda cha saruji cha Mtwara kabla ya kustaafu mwishoni mwa mwaka ujao.
Tayari mwishoni mwa Mei mwaka jana, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa kiwanda hicho mbele ya uongozi wa Mkoa, mawaziri na mabalozi kutoka nchi za Urusi, Misri, Angola, Nigeria na Kenya.
Pinda alisema ujenzi wa kiwanda hicho ni mchango mkubwa kwa maendeleo ya Taifa kwa kuwa sekta ya ujenzi inachangia katika kasi ya ukuaji wa uchumi.
“Mahitaji ya saruji nchini kwa sasa ni tani milioni tatu na viwanda vinne vilivyopo nchini kwa sasa vinazalisha tani milioni 1.2 sawa na mifuko 70,000 kwa siku, kiasi ambacho ni kidogo sana,” alisema Waziri Mkuu.
Aidha, alisema kiwanda hicho kitazalisha tani milioni tatu kwa mwaka sawa na mifuko 150,000 kwa siku na kutoa ajira za moja kwa moja 1,000 na ajira zisizo za moja kwa moja 9,000.
Waziri Mkuu alisema viwanda vilivyopo nchini vinakabiliwa na changamoto mbalimbali kama kukosekana kwa umeme wa uhakika, malighafi ya mawe ya chokaa ambayo huhitajika kwa asilimia 80 kwenye uzalishaji, gesi ya kuyeyusha mawe hayo na kwamba gharama kubwa ya saruji inasababisha isinunulike.
Alisema kutokana na kugundulika kwa gesi asilia mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Lindi na Mtwara, itakuwa maalum kwa ajili ya viwanda vya saruji, kwa kuwa malighafi muhimu ya gesi na mawe inapatikana kwa uhakika hasa mkoani humo katika Kijiji cha Msijute.
Alisema iwapo saruji itapatikana italeta mabadiliko makubwa kwani wananchi wa mkoa huo watainunua kwa bei rahisi na kujenga nyumba za kisasa.
Pinda alisema kampuni zingine 51 zimewasilisha maombi ya kuwekeza mkoani humo katika Kituo cha Uwekezaji (TIC).
Kampuni hizo na idadi ya miradi kwenye mabano  ni mitambo ya luninga na redio (3), kilimo (2), usindikaji korosho (7), majengo ya kampuni na ofisi (2), majisafi (2), bidhaa zitokanazo na saruji (3), mbolea (1), mikate (1), matangi ya mafuta (2), kiwanda cha ujenzi wa maboti (1), mbao (1), utalii (14), uchimbaji na watafutajia wa mafuta (1), usafirishaji (8) na plastiki (1).

No comments: