Wananchi
wa Malawi, leo wanapiga kura kuchagua rais atakayeiongoza nchi hiyo kwa kipindi
kingine cha miaka mitano. Kadhalika, watachagua wabunge na madiwani.
Hii
ni mara ya kwanza kwa wananchi wa Malawi kupiga kura tatu. Chaguzi za nyuma
zilihusisha urais na ubunge pekee huku uchaguzi wa madiwani ukifanywa siku
tofauti.
Katika
siku za kuelekea uchaguzi wa leo, wagombea urais ambao ni 12 walikuwa wakifanya
kampeni katika maeneo mbalimbali ya nchi hadi usiku ili kuvutia wapiga kura.
Taratibu za Malawi zinaruhusu kufanya kampeni hadi usiku.
Kura
za maoni za karibuni zilizotafitiwa na taasisi ya Afrobarometer zilionesha
kwamba wagombea wanne wakubwa wanaowania urais wa nchi hiyo na kupewa nafasi
kubwa ya kushinda wanazidiana kidogo sana.
Wagombea
hao wanne ambao mmoja wao anatarajiwa kuwa rais kutokana na kura za leo ni
Lazarus Chakwera wa chama cha upinzani cha Malawi Congress Party (MCP), Atupele
Muluzi wa chama cha United Democratic Front (UDF), Peter Mutharika wa
Democratic Progressive Party (DPP) na Rais wa sasa wa nchi hiyo, Joyce
Banda anayetokea chama tawala cha People’s Party (PP).
Takriban
vyama hivyo vinne vikubwa vinavyotazamiwa kutoa rais vilishawahi kuongoza nchi
hiyo huko nyuma na takriban vyote, wakati wa kampeni vilijikita katika
kudhamiria kuondoa umaskini na njaa kupitia kilimo na kuongeza ajira kwa
vijana.
Wagombea
wote hawajawahi kugombea nafasi kubwa kama hiyo isipokuwa Rais Joyce Banda,
maarufu kama JB (kifupi cha majina yake), katika uchaguzi wa mwaka
2009 alikuwa mgombea mwenza wa Rais wa zamani wa nchi hiyo, Bingu wa
Mutharika.
Hata
hivyo, JB aliamua kuunda chama chake cha kisiasa baada ya kushindwa kuiva na
rais Bingu wa Mutharika, ingawa aliendelea kuwa Makamu wa Rais
'kiubishiubishi'.
JB
ambaye ni mke wa Jaji Mkuu mstaafu wa Malawi, Richard Banda, alitawazwa kuwa
rais kufuatia kifo cha Mutharika mwaka 2012 kwani katiba ya Malawi inasema
Makamu wa Rais ashike nafasi hiyo kama kitatokea kifo cha Rais.
Mgombea
urais wa DPP, Profesa Peter Mutharika ni mdogo wa Hayati Bingu wa Mutharika
wakati Atupele Muluzi ambaye ana miaka 35 na hivyo kuwa mgombea urais kijana
zaidi kuwahi kutokea nchini humo ni mtoto wa Rais wa zamani wa nchi hiyo,
Bakili Muluzi.
Dk
Chakwera ni sura mpya ambayo chama kilicholeta uhuru wa nchi hiyo kupitia kwa
hayati Dk Kamuzu Banda cha Malawi Congress Party kimemsimisha mwaka huu. Huko
nyuma, chama hicho kilikuwa kikimsimamisha mkongwe wa siasa nchini humo, John
Tembo, lakini alikuwa hafanyi vizuri. Kabla ya kuingia kwenye siasa, Chakwera
alikuwa mchungaji na Rais wa Kanisa la Assemblies of God.
No comments:
Post a Comment