Serikali imesema imetimiza ahadi ya kujenga makaburi ya marehemu Shehe Yahya Hussein na Shehe Kassim Bin Juma, yaliyovunjwa na watu wasiojulikana wakati wa 'Operesheni Safisha Jiji' hivi karibuni kwa Sh milioni 3.9.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadik alisema Manispaa ya Ilala ilipewa kazi ya kujenga makaburi hayo na baada ya kukadiria gharama za ujenzi, walitaka zaidi ya Sh milioni 9.7, lakini haikukubaliwa.
Alisema baada ya familia za marehemu hao kusikia gharama hizo, hawakukubali na kueleza kuwa makaburi ya Kiislamu, hayajengwi kifahari kiasi hicho na kuamua kutafuta mjenzi wao.
Alisema walipomleta mjenzi huyo, alikadiria gharama hiyo ya Sh milioni 3.9, ambapo mjenzi huyo alikubalika na kupewa fedha hizo na kuanza ujenzi wa kaburi la Shehe Kassim Bin Juma.
Sadik alisema kaburi hilo, limejengwa na kumalizika kwa kiwango cha hadhi ya shehe huyo, ambacho familia imeridhia, kisha kuanza ujenzi wa kaburi la pili.
Alisema mjenzi
alipoanza kujenga kaburi la Shehe Yahya Hussein na kufika kozi ya tatu, watoto
wa marehemu huyo, walifika na kusimamisha ujenzi, kutaka wapewe fedha ili
wajenge wenyewe.
Alisema watoto hao, walitaka Sh milioni 4.5 kwa mujibu
wa makadirio ya awali ya Manispaa. Lakini
alisema serikali haikuahidi kuwapa pesa, bali kujenga makaburi.
“Tumefanya hivyo na jana (juzi), nimeenda kuwatembelea
pale na kumuagiza fundi kuendelea na ujenzi, kwani hatukuwa na ahadi ya kuwapa
fedha na kama wakikataa, ni kwa ridhaa yao,” alisema.
Alisema kuna upotoshaji wa suala hilo
unaoendelea, jambo ambalo sio zuri.
Alisema serikali imetimiza ahadi yake ya
kujenga makaburi ya marehemu hao, yaliyovunjwa.
Usiku wa Aprili 10 mwaka huu katika viwanja vya Makaburi ya Tambaza,
jirani na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, makaburi hayo yalivunjwa na watu
wasiojulikana, wakati wa 'Operesheni Safisha Jiji' na serikali kuamua kuyajenga
upya.
No comments:
Post a Comment