MAJAMBAZI WAUA WATATU NA KUPORA FEDHA, VOCHAWatu watatu wameuawa kwa kupigwa risasi na watu wanaosadikiwa kuwa majambazi usiku wa kuamkia jana katika matukio na maeneo tofauti ya wilaya za Kahama na Shinyanga mkoani Shinyanga.
Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga Evaresti Mangala alisema, watu wakiwa na bunduki moja aina ya SMG majira ya saa 1.30 za usiku huko katika mtaa wa Ndala Manispaa ya Shinyanga walimvamia mfanyabiashara Kulwa Cosmas (42) wakati akiwa kwenye ofisi yake ya huduma ya kuweka na kutoa pesa kwa simu.
Katika uvamizi huo majambazi walimpiga risasi shingoni na kusababisha kifo chake papo hapo.
Alisema, siku hiyo hiyo majira ya saa 2.45 watu waliokuwa na bunduki moja ya kivita aina ya SMG walivamia nyumbani kwa mfanyabiashara mwingine Yahaya Mrisho (46)  wakampora Sh 300,000, vocha za simu za kiganjani za mitandao mbali mbali zenye thamani ya Sh 150,000 na simu nne za kiganjani.
Kamanda Mangala alisema, katika tukio jingine lililotokea majira ya saa mbili za usiku huko katika kijiji cha Nyabusalu Kata ya Bulungwa wilayani Kahama watu wasiofahamika walivamia nyumbani kwa mwanamke Milembe Masanja (60) wakati akiwa jikoni na mtoto wake Kulwa Mdirisha (40) wakiandaa chakula cha jioni.
Katika uvamizi huo wavamizi Milembe na mtoto wake Kulwa walipigwa risasi sehemu mbali mbali za miili yao na kusababisha vifo vyao papo hapo na kwamba polisi mkoani hapa inawahoji watu wanne kuhusu tukio la uvamizi wa Ndala.

No comments: