MAHAKAMA YATUPA OMBI LA MBUNGE WA JIMBO LA BAHIMahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imetupilia mbali ombi la Mbunge  Bahi, Omary Badwell (CCM), la kusitishwa kuendelea kusikilizwa kwa kesi  ya kuomba na kupokea rushwa ya Sh milioni nane inayomkabili. 
Badwel kwa aliiomba mahakama hiyo kusimamisha usikilizwaji wa shauri hilo, ili kusubiri uamuzi wa kesi ya kikatiba aliyoifungua Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam.
Akitoa uamuzi huo jana, Hakimu Mkazi, Hellen Riwa, alisema mahakama haitakuwa na sababu ya kutoendelea kusikiliza kesi hiyo kwa kuwa hakuna jambo lililoelezwa na kufanya shauri hilo kusimamishwa. 
Alisema hakuna maelekezo kutoka ngazi ya juu ya kumuelekeza asitishe kesi pia kesi ya kikatiba, iliyofunguliwa na mshitakiwa kuhoji kifungu cha kisheria haihusiani na  iliyopo mahakamani hapo. 
“Uamuzi wa kesi hiyo inaweza kutolewa wakati kesi hiyo inaendelea au kutumiwa na watuhumiwa wengine katika siku zijazo hivyo sikubaliani na maelezo ya wakili wa Badwel, maombi yake yanatupiliwa mbali,” alisema Hakimu Riwa. 
Hakimu Hellen aliahirisha hiyo hadi Juni 12, mwaka huu, mahakama itakapoendelea kusikiliza mashahidi wa upande wa Jamhuri. Uamuzi , huo ulitolewa wakati  Badwel hakuwepo  mahakamani kwa madai yupo mjini Dodoma anahudhuria vikao vya Bunge. 
Kupitia kwa Wakili wake Mpare Mpoki, Badwell alidai wamefungua kesi hiyo kwa kuwa kifungu hicho kinapingana na Ibara ya 13(6)(a) ya Katiba, ambayo inampa haki mtu yeyote kupinga uamuzi wowote ambao anaona utamuathiri.
Aidha wanaiomba Mahakama Kuu itamke kifungu hicho ni batili na kinapingana na Katiba. 
Inadaiwa kati ya Mei 30 na Juni 2 mwaka 2012, katika maeneo tofauti Dar es Salaam, mshitakiwa alishawishi apewe rushwa ya Sh milioni nane kutoka kwa aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, Sipora Liana. 
Ilidaiwa,  Badwel aliomba rushwa hiyo ili awashawishi wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), kupitisha hesabu za Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani. Pia anadaiwa Juni 2, 2012 katika Hoteli ya Peacock, iliyopo Ilala, alipokea rushwa ya Sh milioni moja kutoka kwa Sipora.

No comments: