Magari
ya iliyokuwa Kampuni ya Usafiri Dodoma (KAUDO) yanatarajiwa kuuzwa hivi
karibuni baada ya kumalizika kwa kesi kati ya mmoja wa waliokuwa wafanyakazi
wake aliyeishitaki Serikali.
Kwa
mujibu wa Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk Charles Tizeba, hukumu ya kesi hiyo
ilitoka mwaka 2011 ambapo Serikali ilishinda.
Alisema
taratibu za Serikali za kupata kibali cha uuzaji wa magari hayo
zimeshakamilika.
“Hivi
sasa, zoezi la kufanya uthamini wa magari hayo linaendelea na linatarajiwa
kukamilika mwishoni mwa mwezi Juni 2014. Baada ya tathimini kukamilika, magari
hayo yatauzwa kwa uwazi na kwa njia ya ushindani,” alisema Dk Tizeba.
Alisema
awali uuzaji wa mali za msingi za shirika hilo hususan magari haukufanyika
kutokana na mmoja wa aliyekuwa mtumishi wa Kaudo kufungua shauri namba 352 la
mwaka 2000 mahakamani akidai kulipwa mafao ya Sh milioni 98.
“Kutokana
na kufunguliwa kwa shauri hilo, mahakama iliweka zuio ya kutouzwa kwa magari
kumi (10) ya shirika hilo hadi hapo shauri litakaposikilizwa na kutolewa
maamuzi,” alisema Dk Tizeba.
Naibu
Waziri alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Lushoto, Dk Henry Shekifu (CCM)
aliyehoji Serikali inachukua hatua gani kunusuru vifaa vya magari ya kampuni
hiyo.
No comments:
Post a Comment