MADIWANI WAPINGA KUSHIRIKI UCHAGUZI NA RAIS, WABUNGE



Wajumbe wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa (Alat), ambao wengi ni madiwani wamepinga utaratibu wa Uchaguzi Mkuu, kutumiwa na wananchi kuchagua rais, wabunge na madiwani.
Kutokana na hatua hiyo, wajumbe hao sasa wamependekeza uchaguzi wa madiwani, utafutiwe wakati mwingine, ili jamii itambue umuhimu wao katika kupatikana kwa ushindi wa wabunge na rais.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa wilaya hiyo, Hamis Said, aliwaambia wajumbe wa Alat kuwa ongezeko la posho za wabunge haliwezi kuachwa likaendelea kufumbiwa macho, huku thamani ya madiwani ikizidi kushuka.
Sababu ya hatua hiyo zilitolewa jana katika Mkutano Mkuu wa Alat, kwamba ni ongezeko la posho ya vikao kwa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania la hivi karibuni na viwango vya posho za wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, vinavyoonekana wao wamedharauliwa. 
Huku akiungwa mkono na kushangiliwa na zaidi ya wajumbe 500 wa Alat,  Said  alisema hakuna maana tena kuendelea kutumika kwa kauli mbiu ya mafiga matatu ambayo hutumiwa  na CCM kwenye uchaguzi, ikiwahamasisha wananchi kumpigia kura rais wa CCM, mbunge wa CCM na diwani wa CCM, wakati baada ya uchaguzi madiwani hupuuzwa.
“Kuanzia sasa wao wawe na uchaguzi wao na sisi tuwe na uchaguzi wetu. Haiwezekani kazi kubwa tunafanya sisi kule kwenye mitaa, vitongoji, kata na tarafa lakini baada ya kuisha uchaguzi wanaangalia maslahi yao tu, sisi tukibakia taabani.
“Tumeshuhudia wabunge wa Katiba wakilipwa Sh 300,000 za vikao. Juzi juzi Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wanaanza vikao vya bajeti,  wameanza na posho mpya ya Sh 300,000. Yaani mtu alikuwa hana kitu lakini anaanza na kiwango kikubwa cha fedha, sisi watendaji wa Serikali za Mitaa ambao ndio tunahangaika na  wananchi tunapuuzwa,”  alisema.
Hata hivyo hasira za wajumbe hao ambao wengi ni madiwani, wenyeviti wa halmashauri za wilaya na mameya dhidi ya ongezeko la posho hizo za wabunge zinaweza kuisha wakati wowote kutokana na ahadi ya juzi ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ambaye ameahidi  kuwa Serikali itapandisha posho za madiwani katika bajeti ya mwaka huu wa fedha.
Pinda alisema hivyo alipokuwa akijibu kilio hicho cha posho finyu ya madiwani, ambacho awali kiliwasilishwa na Mwenyekiti wa Alat Taifa, Dk Didas Masaburi,  kwa Pinda alipozindua Mkutano huo wa 30 wa Alat juzi.
Akijibu hoja hiyo, Pinda alisema alichofurahishwa na maombi ya juzi ya Alat  kutaka madiwani kuongezewa posho ilikuwa ni hatua ya maombi hayo kutoshinikiza kiwango fulani kama ambavyo wamekuwa wakishinikiza miaka ya nyuma.

No comments: