MADENI YA WALIMU YAGEUZWA 'MRADI'


Rais Jakaya Kikwete, amesema Serikali imebaini kuwepo kwa mchezo mchafu unaotumiwa na baadhi ya watumishi wasio waaminifu,  unaosababisha malimbikizo ya madeni ya wafanyakazi hususani walimu kutomalizika, kwa maslahi yao binafsi.
Amesema watumishi hao wamekuwa wakitumia fursa hiyo ya madai hasa ya walimu na kurejesha Hazina madeni hata yaliyolipwa, huku walimu wenyewe wakiwa hawana taarifa jambo linalofanya kuwepo na mkanganyiko wa takwimu halisi za deni la malimbikizo ya walimu hao.
Alisema hayo jana katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani, ambapo awali wakati wafanyakazi hao wakipita mbele yake na maonesho ya kazi zao, walimu wakiongozwa na Chama  cha Walimu (CWT), walipita mbele yake, na kudai malimbikizo ya mishahara, likizo na uhamisho.
“Mashemeji zangu kama mlivyoniita leo nawahakikishia tumeshabaini mzizi wa fitina, Serikali imekuwa ikijitahidi kuhakiki madeni yenu ili kukamilisha malipo, lakini kwa mshangao tumegundua deni halisi si Sh bilioni 19, ni kama Sh bilioni tisa tu, kuna wajanja wanajinufaisha kupitia migongo yenu,” alisema Rais Kikwete.
Alisema imebainika kuwa wapo walimu wengi wameshalipwa malimbikizo yao, lakini majina yao na madeni yamerejeshwa upya Hazina huku walimu wenyewe wakiwa hawana taarifa na watu wanaofanya hivyo wakiwa hawajulikani.
“Nimeshaielekeza Wizara ya Fedha na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, kuchunguza kwa kina ili wakaguzi na wahasibu wasio waaminifu wanaofanya mchezo huu mchafu wabainishwe na kuchukuliwa hatua,” alisema.
Alisema kwa sasa Serikali inaendelea na kazi ya kuhakiki madeni ya watumishi wasio walimu, ambapo kati ya halmashauri 147 tayari, halmashauri 96 zimehakikiwa na madeni yameanza kulipwa na halmashauri 51 zilizobaki zikiwa katika hatua ya kuanza kuhakikiwa.
Awali wakati maadhimisho hayo yanaanza, yalitawaliwa na nderemo na vifijo kutoka kwa wafanyakazi waliojitokeza kwa wingi kuandamana na kupitisha bidhaa na kazi zao mbele ya Rais na viongozi wa kitaifa.
Katika maandamano hayo, walimu wakiongozwa na CWT walipofikia jukwaa la Rais Kikwete walisimama huku wakicheza na kuimba walisikika wakiimba; “shemeji mshahara bado” jambo lililomshitua Rais Kikwete ambaye alilazimika kufuatilia papo hapo na kugundua mshahara wa mwisho wa mwezi uliopita umechelewa.
Hata hivyo alifafanua tatizo lilivyotokea kwa kuwa kutoka Benki Kuu mishahara hiyo ilishatoka na kuahidi kuwa halitatokea tena. 

No comments: